Je wajua waweza kujifunza kitu chochote kwa saa 20 tu?

Je wajua waweza kujifunza kitu chochote kwa saa 20 tu?

Like
642
0
Monday, 17 December 2018
Global News

Iwe Kirusi, Kiarabu ama Kichina, au hata fizikia ya maumbo. Ubongo wa binaadamu unaweza kujifunza kitu chochote kile, hata kiwe kigumu namna gani, tena kwa haraka.

Utafiti unaonesha kuwa muda bora kabisa wa kujifunza kitu ni saa 20 za awali unapokutana na somo ama ujuzi mpya.

Wakati huo ndio kasi ya ubongo kupata uelewa ni kubwa zaidi. Kutokana na hamu ya kung’amua mapya, uwezo wa ubongo kufahamu nao huwa mkubwa.

Mwanafalsafa wa karne ya 19 nchini Ujerumani Herman Ebbinghaus ambaye pia alikuwa ni mwanasaikolojia ni moja ya wasomi wa mwanzo ambao walitafiti juu ya namna ubongo unavyokusanya taarifa mpya.

Kulielezea hilo, Ebbinghaus alitengena kile alichokiita learning curve, yaani mchirizo wa kujifunza: ama uhusiano kati ya kupata stadi mpya na muda utumikao kujifunza.

Mchirizo huo una mihimili miwili wa wima ama y ni wa maarifa na mhimili mlalo ama y ni wa muda.

Ebbinghaus aligundua kuwa kwa saa chache za mwanzo muda mwingi zaidi ukitumika kujifunza somo jipya na ndivyo hivyo maarifa zidi hupatikana.

Lakini baada ya muda kasi ya kujifunza huanza kushuka: japo ukiendelea kujifunza utapata uelewa zaidi lakini si kwa kasi kama ya saa 20 za mwanzo.

Katika wakati huu wa sasa, njia hiyo iliyobuniwa na Ebbinghaus inatumika kama kipimo cha kufahamu muda muafaka wa mtu kujifunza ujuzi mpya, na katika ulimwengu wa biashara hutumika kupima kasi ya utendaji kazi.

Ubongo wa binaadanu unaweza kujifunza kitu chochote kile, hata kiwe kigumu namna gani, tena kwa haraka.

Saa 20 za mwanzo ndizo muhimu zaidi kwenye kujifunza kutokana na hamu ya ubongo kuwa juu, lakini kadri ubongo unavyozidi kung’amua somo hilo ndivyo pia unavyochoka na kufanya kasi ya kujifunza kupungua.

Ndio maana hata somo liwe gumu namna gani, athari kubwa zaidi za kuelewa hutokea mwanzoni na kwa haraka kabla kasi kupungua.

Tafuta mbinu yako ya kujifunza

Josh Kaufman, mtunzi wa vitabu kutoka Marekani ni muumini wa nguvu ya kujifunza haraka kwa saa za mwanzoni.

Kigezo hicho ndiyo kilikuwa msingi wa kitabu chake maarufu ‘The First 20 Hours: Mastering the Toughest Part of Learning AnythingSaa 20 za Mwanzo: Kuhimili sehemu ngumu ya kujifunza kitu chochote.

 

Ushauri wake ni kuwa, vunja vunja somo katika vipande vinavyoweza kumeng’enyeka, na jikite katika kujifunza vipande hivyo kwa dakika 45 kwa siku, kila siku.

Hautakuwa mahiri au gwiji lakini utakapokamilisha saa 20 zako za mwanzo za kazi ngumu (ambazo utazifikisha baada ya mwezi) utakuwa umepata ufahamu wa kutosha wa somo hilo.

Na pale utakapokuwa na ufahamu wa kutosha, njia ya kuwa mbobezi inakuwa nyeupe.

Njia nyengine inayopigiwa upatu ni kanuni ya saa tano ama ‘Five-Hour Rule’: ambapo mtu hutakiwa kutenga saa moja kujifunza kitu kipya katika siku tano za wiki.

Benjamin Franklin, ambaye ni moja ya waanzilishi wa taifa la Marekani alikuwa ni mmoja ya wale waliokuwa wakiutumia mfumo hou na kuupigia chapuo kwa wengine. Mfumo huo pia huitwa kujifunza kwa dhamira.

Franklin alikuwa akipanga kila siku kuanzia Jumatatu mpaka Ijumaa saa moja kujifunza kitu kipya.

Na pale alipoona kuwa ameshapata uelewa wa kutosha alihamia kwenye somo jipya. Alifanya hivyo maisha yake yote.

Kwa mujibu wa wataalamu, iwapo utatumia njia hii ya kujifunza, utapata uelewa na stadi mpya katika kila wiki nne maishani mwako. Cha muhimu zaidi ni kuwa na muendelezo na ari.

Nadharia ya kujifunza kwa dhamira inatumiwa na maelfu ya watu duniani.

Baadhi ya watu mashuhuri na wafanyabiashara wakubwa duniani wameitaja njia hiyo kama siri yao ya mafanikio. Oprah Winfrey, Bill Gates, Elon Musk, Warren Buffett na Mark Zuckerberg ni miongoni mwa watu wanaotumia mfumo huo wa kujifunza.

Ukitaka kupata maarifa na stadi mpya kunahitajika vitu viwili vikuu: ari ya kujifunza na nidhamu binafsi ya kujisukuma ili utende uyatakayo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *