Jiwe lililotokana na ‘taa ya wachawi’

Jiwe lililotokana na ‘taa ya wachawi’

1
1750
0
Tuesday, 23 October 2018
Local News

Kupiga picha kwenye kimondo cha Mbozi ni tukio la kipekee kwenye kivutio cha utalii kilichopo wilayani Mbozi, mkoa wa Songwe, Nyanda za Juu Kusini nchini Tanzania.

“Wengi huwa wanafurahia kupiga picha kwa sababu ni kitu cha kipekee na tunaamini kuwa mtu akishapiga picha anakuwa balozi wa kimondo hiki kwa wengine,” anasimulia Beatus Bonabana, Mhifadhi, kivutio cha Kimondo Mbozi, anaongeza akisema.

‘Katika miaka ya nyuma, wenyeji wa eneo hilo walikuwa wanakitumia sehemu hiyo kwa ajili ya maombi ya kupata kitu, walifanya matambiko, ni jambo linaloendelea kufanyika mpaka leo.”

Kimondo cha Mbozi kinakadiriwa kuwa na uzito wa tani 12 na ni cha nane kwa ukubwa duniani.

Ni cha pili Afrika baada ya kimondo cha Hoba chenye tani 60. Kimondo cha Hoba kilichopo nchini Namibia ndicho kikubwa zaidi Afrika na duniani.

Haijulikani ni lini hasa kimondo hiki cha Mbozi kilianguka, ila mtu wa kwanza kukiona katika miaka ya 1930 alijulikana kwa jina la Halele Simbaya, ambaye alikuwa mhunzi.

Halele alipogundua kimondo hiki alitoa taarifa kijijini kwao, ndipo wenyeji wakaanza kuabudia katika shimo ambalo huwa linahifadhi maji ambayo wenyeji hunawa kupata baraka na wakalita jambo hilo kuwa ni kusafisha nyota.

“Wenyeji walikuwa wanakatakata kimondo hicho, wakaita kipande cha nyota na hata sasa wenyeji wanakiita kimondo cha nyota. Watu walikata ili kusafisha nyota, ulinzi ulipowekwa ilisaidia,” Bonabana alieleza.

Zamani kimondo hiki kilikuwa kinang’aa lakini sasa kimekuwa na rangi nyeusi baada ya kuathiriwa na hali ya hewa.

Kimondo hiki hakifanani na chuma aina nyingine kutokana na ugumu wake na ukikipiga ni kama kuna uwazi ndani yake, unasikika mlio wa sauti ambao ni tofauti.

Sauti inayoonesha kuwa ndani kuna uwazi na hii inatokana na madini ambayo yaliyokiumba.

Imani kuhusu kimondo haipo miongoni mwa wenyeji hao wa Mbozi tu, bali sehemu mbali mbali duniani ambako vinapatikana.

Wenyeji wake huhusisha zaidi na nguvu za Kimungu, hivyo kuyafanya maeneo vilipoangukia kuwa maeneo matakatifu kwa misingi ya imani zao.

Mambo matatu kukihusu kimondo cha Mbozi

  • Kimondo cha Mbozi kinakadiriwa kuwa na uzito wa tani 12
  • Ni cha nane kwa ukubwa duniani
  • Cha pili Afrika baada ya kimondo cha Hoba chenye tani 60.
  • Inaaminika mtu wa kwanza kukiona katika miaka ya 1930 ni Halele Simbaya.
  • Hakipati joto la jua kali hata katika msimu wa kiangazi.

Inaelezwa kuwa tangu zama za kale, vimondo viliaminika kuwa vitu vitakatifu na jamii mbali mbali za wakati huo duniani.

Utaratibu wake wa kuanguka hapa duniani, ambapo huambatana na mwanga na sauti, kama vile nyota idondokayo, vumbi na kishindo imekuwa siku zote ikisababisha hofu kwa wale walioshuhudia.

Sifa za kimondo cha Mbozi

Kimondo hiki huwa ni baridi wakati wote, hata wakati wa msimu wa kiangazi ambapo jua huwa kali sana, lakini bado huwa cha baridi.

Hiki ni kimondo kikongwe duniani kwa sababu hata hakijajulikana kilianza kuwepo hapo tangu lini tofauti na vimondo vingine duniani vinajulikana vilianguka lini (tarehe au mwaka) au kuonekana athari zilizosababishwa na kuanguka kwa kimondo hicho.

Mfano kimondo kikianguka na kugongana na uso wa ardhi huwa kinaharibu makaazi ya watu au kama ni msituni miti pia huvunjika na kina tabia ya kujichimbia.

Mfano kimondo kikubwa duniani ambacho kipo Namibia, kilipogonga uso wa ardhi kilijifukia.

Sayansi na watafiti wanasema kimondo kikiwa na uzito wa zaidi ya tani 100 huwa kinalipuka na hufika duniani kikiwa vipande vipande.

Kimondo cha Mbozi ndicho kikubwa kwa Tanzania, hata hivyo vipo vingine saba vidogo, hivi vinabebeka na vimehifadhiwa katika makumbsho ya taifa, Dar es salaam.

Kwa nini Kimondo ni kivutio cha utalii?

Kimondo ni kitu cha kipekee kwa sababu kimetoka nje ya anga ya dunia.

Vitu hivi vimetokea sayari nyingine ya Mars na Jupita.

Vitu hivi vimetokea katika mvuto wa jua na sayari zingine.

”Mfano mzuri wa kimondo ni vile tunavyoviona kama taa inayokimbia angani, vijijini huwa tunaita taa za wachawi wakati si kweli ni vimondo.

Vile huwa ni vimondo vidogo vinavyoishia hewani na ndio mfano wa kimondo kama hiki,” anasimulia mhifadhi.

Watalii wanaotembelea eneo hilo, ni wale tu wenye lengo la kukiangalia na kupiga picha, ambao hata hivyo sio wengi.

Wadau wa utalii wanabainisha kuwa endapo eneo hilo litakuwa na kituo cha utafiti kuhusu masuala ya unajimu na makumbusho litakuwa eneo muhimu sana kwa watalii wa nje na ndani, hususani wanafunzi, hivyo kuwa kitovu cha elimu hiyo ya unajimu.

Takwimu katika kituo hicho zinaonyesha kuwa wastani wa wageni wanaotembelea hapo ni kati ya 250 mpaka 350 kwa mwaka na wengi huwa ni wanafunzi.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *