RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia Salamu za Rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mheshimiwa Ali Nasoro Rufunga kuomboleza vifo vya watu 38 huku wengine 82 wakijeruhiwa usiku wa kuamkia jana tarehe 4 Machi, mwaka huu.
Tukio hilo la kusikitisha limetokea katika Kata ya Mwakata iliyoko katika Wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga kufuatia mvua kubwa ya mawe iliyonyesha ikiambatana na upepo mkali, hivyo kuathiri watu 3,500.
Katika Kata Mwakata iliyoathiriwa zaidi, kaya 350 zimeathiriwa katika Kijiji cha Makata wakati katika Kijiji cha Ngumbi, kaya 100 zimeathirika. Katika Kijiji cha Magung’hwa, kaya 50 pia zimeathiriwa..
Rais Kikwete amesema msiba huo siyo wa Wana-Shinyanga pekee bali ni wa Taifa zima ambalo limepoteza nguvukazi muhimu kwa maendeleo yake na ustawi wa jamii ya Watanzania kwa ujumla.