Mahakama Kuu nchini Kenya imeamuru mwanamke aliyeteswa na kudhalilishwa wakati wa kujifungua hospitalini alipwe fidia ya jumla ya dola 25,000 za Marekani.
Mwanamke huyo alidhalilishwa miaka mitano iliyopita katika kisa ambacho kilizua lalama kutoka kwa raia na watetezi wa haki za kibinadamu baada ya kuangaziwa kwenye vyombo vya habari na mtandaoni.
Jaji wa mahakama kuu ya Bungoma, magharibi mwa Kenya, Abida Aroni alisema mamlka ya afya nchini Kenya ilikiuka haki za kimsingi za Josephine Majani alipotengwa na kukosa kuhudumiwa wakati wa kujifungua katika hosipitali ya umma mwaka 2013.
Jaji huyo alisema kuwa haki za kimsingi za afya za Bi Majani, pamoja na heshima yake vilikiukwa kupitia yeye kuteswa kimwili na kutusiwa na wauguzi katika hospitali ya Bungoma.
Na kutokana na hilo, akaamuru alipwe fidia ya dola alfu 25.
Bi Majani amefurahia uamuzi huo akisema kuwa haki hatimaye imetendeka.
Aliyoyapitia Josephine mikononi mwa wauguzi hao yalipata kujulikana baada ya mtu kurekodi video kwenye simu yake na kuipakia kwenye mtandao wa kijamii.