Kabila haondoi uwezekano wa kugombea tena urais baadaye

Kabila haondoi uwezekano wa kugombea tena urais baadaye

Like
522
0
Monday, 10 December 2018
Global News

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo anayeondoka madarakani Joseph Kabila amesema haondoi uwezekano wa kugombea tena urais mwaka 2023

Katika mazungumzo ya nadra na vyombo vya habari, Rais Joseph Kabila ameliambia shirika la Associated Press (AP) kwamba anatarajia kuendelea kutoa mchango katika kushughulikia matatizo yanayoikumba Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo hata baada ya uchaguzi wa Desemba 23 ambao utaamua mrithi wake.

Kabila ameiambia AP kwamba amejitahidi ”kadri ya uwezo wetu” kwa maslahi mema ya Congo tangu alipoingia madarakani mwaka 2001 kufuatia kuuwa kwa baba yake. Hata hivyo, kiongozi huyo alisema bado yapo mengi ya kufanya.Alipoulizwa ikiwa anaweza kugombea tena urais, kwa tabasamu Kabila amejibu ”siwezi kuondoa uwezekano wa chochote maishani.”

Hofu ya utawala wa kupita mlango wa nyuma

Kauli kama hiyo ya Kabila inawatia hofu wapinzani nchini Congo, wanaodhani kwamba Kabila mwenye umri wa miaka 47 ataendelea kuiongoza nchi kupitia mlango wa nyuma, ikiwa mtu aliyemteua kuwa mrithi wake, Emmanuel Ramazani Shadary atashinda uchaguzi mkuu ujao.

Joseph Kabila amesema hofu kama hizo hazina msingi, kwa sababu katiba ya nchi yaiachi mwanya wa jambo hilo kutokea. Hata hivyo, rais huyo amechaguliwa kuwa kiongozi wa kimaadili wa muungano wa kisiasa ulioundwa hivi karibuni, ukijulikana kama ”Common Front for Congo”, nafasi inayombakisha karibu na madaraka ya nchi.

Katiba ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo inamruhusu Kabila kugombea tena, kwa sababu inachokataza ni kuongoza mihula mitatu ya urais, mfululizo. Lakini yeye anasema kwa sasa atabaki kuwa mtu wa kutoa ushauri kwa yule atakayetaka kushauriwa. ”Nina matumaini watanijia kutaka ushauri,” ameiambia AP.

Kumbukumbu ya Mobutu

Uwezekani wa Joseph Kabila kurejea tena madarakani unawakumbusha Wakongo utawala wa mua mrefu wa dikteta Mobutu Sese Seko, ambaye alidumu madarakani kwa miongo mitatu.

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, mojawapo ya nchi kubwa kabisa kieneo barani Afrika na yenye utajiri mkubwa wa maliasili haijawahi kushuhudia ubadilishanaji wa madaraka kwa njia ya amani tangu ilipopata uhuru wake kutoka Ubelgiji mwaka 1960.

Uchaguzi wa mwishoni mwa mwaka huu umecheleweshwa kwa tariban miaka miwili, hali iliyomruhusu Joseph Kabila kuendelea kukaa madarakani baada ya mihula yake miwili kumalizika.  Kwa wanaokosoa kuchelewa huko, Kabila anasema Congo yenyewe ni changamoto, na kuandaa uchaguzi katika nchi hiyo ni changamoto kubwa zaidi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *