Kangi Lugola Atoa Onyo Makampuni ya Ulinzi Yanayoajiri Vikongwe

Kangi Lugola Atoa Onyo Makampuni ya Ulinzi Yanayoajiri Vikongwe

Like
618
0
Monday, 06 August 2018
Local News

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Alphaxard Lugola, ametoa mwezi mmoja kwa makapuni binafsi ya ulinzi nchini kuhakikisha yanarekebisha mfumo wao wa kuajiri pamoja na utoaji wa mishahara kabla ya Wizara yake haijaanza kuyahakiki makampuni hayo.
Lugola amesema baadhi ya Makampuni hayo yameajiri wazee wasiojiweza ambao muda wote wanalala na wanasabaisha uhalifu kuendelea kwa kasi, wakati vijana wapo wengi wenye nguvu zao wanaweza wakazifanya kazi hizo kwa umakini zaidi, na pia tatizo lingine wanalipwa mishahara midogo hali hiyo inawafanya pia wajiingize katika uhalifu.
Akizungumza na mamia ya wananchi mjini Bunda, mkoani Mara katika mkutano wa hadhara uliofanyika Stendi ya zamani mjini hapo, Waziri Lugola alisema, Serikali ya awamu ya tano kamwe haitataka uzembe, hivyo makampuni hayo yanayovunja utaratibu huo siku zao zinahesabika.
Lugola aliongeza kua, licha makampuni hayo yamekua yakiwekeza nchini na pia yanasaidia kufanya doria katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo ya miji, lakini yapo maeneo machache baadhi ya makampuni yanavunja sheria ya nchi kwa kufanya mambo kinyume na sheria inavyowaelekeza.
“La kwanza kabisa makampuni haya yanafanya mambo ya hovyo kwa kuajiri vikongwe kufanya kazi za ulinzi, utamkuta kikongwe kavaa sare ukimuuliza anasema mimi ni mfanyakazi wa kampuni fulani, hii haikubaliki hata kidogo, kwasababu kwa umri ule hawawezi kupambana na wahaarifu, na kwa umri ule muda wote usinzia na baadhi yao unyang’anywa silaha,” alisema Lugola.
Pia lugola alisema kitendo cha baadhi ya makampuni hayo kulipa mishahara midogo, au kutowalipa kabisa wafanyakazi hao, hiyo hali inasababisha uhalifu kwasababu wafanyakazi hao hawataridhika na kipato duni hivyo uweza wakashirikiana na wahalifu au wenyewe kushiriki matukio hayo.
“Nataka makampuni haya yajirekebishe na yasipojirekebisha ndani ya mwezi mmoja ambapo tunataka kuyaakiki makampuni haya, wasije wakamlaumu waziri wa mambo ya ndani ya nchi ambapo yapo baadhi ya makampuni tutaondoa tulichoridhia ili wasifanye kazi katika nchi hii,” alisema Lugola.
Aidha, Lugola aliwataka askari polisi nchini wahakikishe wanafanya kazi kwa weledi na endapo askari atawaonea wananchi kwa kuwabambikizia kesi, kuwaomba rushwa, ameapa katika uongozi wake atahakikisha anawaondoa.
Pia Lugola aliwataka madereva wa magari yakiwemo mabasi pamoja na bodaboda kua makini kwa kufuata sheria za barabarani kwa kuwa, Rais John Magufuli wakati anamuapisha aiongoze wizara hiyo, alisema amechoshwa na ajali zinazotokea nchini ambazo zinamfanya atoe rambirambi kila siku, hivyo yeye kama Waziri husika, hatakubali kuona madereva wanafanya uzembe barabarani.
Katika mkutano huo ulioandaliwa na ofisi ya mkuu wa wilaya, ulihudhuriwa na viongozi wa wilaya hiyo pamoja na mamia ya wananchi wa Bunda ambapo baadhi ya wananchi walipewa nafasi ya kumuuliza maswali Waziri huyo. Hata hivyo, Waziri Lugola aliyajibu maswali hayo ambapo baadhi ya maswali yalililalamikia Jeshi la Polisi Bunda, baadhi ya askari wanawanyanyasa wananchi, Lugola aliyajibu maswali yote katika mkutano huo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *