Kiboko cha mbu wa malaria chapatikana

Kiboko cha mbu wa malaria chapatikana

Like
865
0
Friday, 31 May 2019
Slider

Ukungu (fangasi) – ambao umeboreshwa kisayansi kutoa sumu ya buibui – unaweza kuua idadi kubwa ya mbu wanaoambukiza malaraia, utafiti mpya wa kisayansi umebaini.

Majaribio ya ukungu huo, ambayo yamefanyika nchini Burkina Faso, Afrika Magharibi yameonesha kuwa idadi ya mbu iliteketezwa kwa 99% ndani ya siku 45.

Watafiti wanasema si lengo lao kutokomeza mbu hao bali kusaidia kuzuia maambukizi ya malaria.

Ugonjwa wa malaria, unaoambukizwa na mbu jike aina ya Anopheles wanyonyao damu huua zaidi ya watu 400,000 kwa mwaka.

Duniani kote, wagonjwa milioni 219 wa malaria kila mwaka huripotiwa.

Utafiti huo umefanywa na wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Maryland cha Marekani – na kituo cha utafiti cha IRSS cha Burkina Faso.

Wataalamu hao kwanza walianza kwa kutambua kuvu ama ukungu aina ya Metarhizium pingshaense ambao kiasili kudhuru mbu waambukizao malaria.

Hatua iliyofuatia ilikuwa ni kuuongezea nguvu ukungu huo.

“Kuvu hiyo ni rahisi kuiongezea kitu kisayansi, hivyo ni rahisi kuifanyia uhandisi jeni,” amesema Profesa Raymond St Leger, kutoka Chuo Kikuu cha Maryland.

Wanasayansi hao wakageukia sumu itokanayo na aina ya buibui wa funnel kutoka Australia.

Vipimo vya maambara vikathibitisha ufanisi wa kiwango cha juu cha sumu hiyo katika kuteketeza mbu.

Baada ya maabara, wataalamu hao wakatengeneza kijiji maalum kwa ajili ya utafiti nchini Burkina Faso.

Kijiji hicho kilizungushiwa neti ili kuzuia ukungu ama mbu kutoka kwenye eneo la utafiti.

Ukungu huo kisha ukachanganywa na mafuta ya ufuta na kumwagiwa kwenye mashuka meusi ya pamba.

Mbu hao walidhurika punde tu walipotuwa kwenye mashuka hayo.

Watafiti walianza kazi hiyo na mbu 1,500.

Matokeo ya utafiti huo, yaliyochapishwa kwenye jarida la kisayansi yalionesha kuwa idadi ya mbu inaongezeka kama wakiachwa bila ya ukungu.

Ila, baada ya ukungu wenye sumu kuingizwa kwenye kijiji hicho, walisalia mbu 13 tu baada ya siku 45.

Aina mpya za kupambana na malaria zinahitajika kwa haraka duniani, kutokana na mbu hao kutengeneza usugu wa dawa.

Shirika la Afya Duniani (WHO) tayari limeshaonya kuwa idadi ya wagonjwa itaendelea kuongezeka kwenye nchi 10 ambazi zimeathirika zaid na malaria barani Afrika.

 

cc;BBCswahili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *