Kim Jong-un atishia kufuta mkutano wake na Trump

Kim Jong-un atishia kufuta mkutano wake na Trump

Like
460
0
Wednesday, 16 May 2018
Global News

Korea Kaskazini imesema huenda ikaufuta mkutano kati ya kiongozi wake Kim Jong-un na Rais wa Marekani Donald Trump iwapo Marekani itaendelea kusisitiza kwamba taifa hilo la bara Asia ni lazima liharibu au kusalimisha silaha zake za nyuklia.

Mkutano huo ambao umesubiriwa kwa hamu kati ya Bw Trump na Bw Kim unatarajiwa kufanyika mnamo 12 Juni.

Hayo yamejiri baada ya Korea Kaskazini kusema imejitolea kuhakikisha silaha za nyuklia zinaondolewa katika rasi ya Korea.

Maandalizi ya mkutano huo wa Trump-Kim yamekuwa yakiendeleza, lakini sasa kumeingia shaka kuhusu hilo.

Shirika la habari la serikali ya Korea Kaskazini KCNA limemnukuu naibu waziri wa mambo ya nje Kim Kye-gwan akisema iwapo Marekani “itatubana na kusisitiza kwamba ni lazima tusalimishe bila masharti silaha zetu za nyuklia basi hatutakuwa tena na hamu ya kushiriki mazungumzo hayo na itatulazimu kutafakari upya iwapo tutakubali mkutano unaotarajiwa kufanyika karibuni kati ya DPRK-US.

Korea Kaskazini kirasmi hufahamika kama Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Korea (DPRK).

Bw Kim amesema Korea Kaskazini “ilikuwa na matumaini makubwa kwamba mkutano huo ungechangia kupunguza wasiwasi katika Rasi ya Korea na kuwa hatua muhimu katika kuunda siku za usoni zenye matumaini makubwa.

“Hata hivyo, inasikitisha sana kwamba Marekani inatuchokoza kabla ya mkutano huo kwa kutoa matamko ya kushangaza.”

Mapema Jumatano, dalili za wasiwasi zilianza kutokea, Korea Kaskazini ilipojiondoa kutoka kwa mazungumzo yaliyokuwa yamepangwa kati ya nchi hiyo na Korea Kusini.

Maafisa wa ngazi ya juu wa mataifa hayo walitarajiwa kukutana katika eneo la mpakani ambapo majeshi hayaruhusiwi kujadiliana maelezo zaidi kuhusu makubaliano ambayo yalikuwa yameafikiwa katika mkutano mkuu kati ya mataifa hayo mwezi uliopita.

Lakini Korea Kaskazini ilijiondoa ikisema imekerwa na mazoezi makubwa ya kijeshi yanayoandaliwa kati ya Korea Kusini na Marekani.

Mazoezi hayo ya kijeshi, yaliyopewa jina Max Thunder yalitarajiwa kufanyika katika kipindi ambacho michezo ya Olimpiki ya majira ya baridi ilikuwa inafanyika, lakini yakaahirishwa baada ya matumaini ya kuimarika kwa uhusiano kati ya Korea Kusini na Kaskazini kutokea.

Korea Kaskazini ilikuwa awali imesema ilifahami kwamba operesheni hiyo ya kijeshi ingeendelea.

Lakini KCNA wamesema sasa kwamba mazoezi hayo ya kijeshi ni “uchokozi” na maandalizi ya uvamizi, jambo linaloashiria kurejelewa kwa lugha kali iliyokuwa inatumiwa wakati wa uhasama kati ya Marekani na Korea Kusini

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *