Kundi la IS kuvamia Mashariki mwa DRC

Kundi la IS kuvamia Mashariki mwa DRC

Like
645
0
Thursday, 23 May 2019
Global News

Wakuu wa vyombo vya usalama katika kanda ya Maziwa Makuu wanakutana nchini Uganda kupanga mikakati ya kukabiliana na tishio la kundi la Islamic State ambalo linasemekana limeanza kuendesha harakati zake katika maeneo ya Mashariki na Kaskazini mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Hayo ni kwa mujibu wa upelelezi wa chombo cha usalama kinachowaleta pamoja wakuu wa usalama katika kanda ya maziwa makuu, kuna uwezekano wa eneo hilo kuingiliwa kirahisi na wanamgambo wa kundi hilo kutokana na ukosefu wa usalama na mlipuko wa ugonjwa wa Ebola ambao unatatiza juhudi za kukabiliana nao.

Vyombo vya usalama katika eneo hilo sasa vinataka kuhakikisha kuwa kundi hilo halipati nafasi kuendesha shughuli zake katika matatifa ya eneo hilo baada ya kutimuliwa mashariki ya kati.

”Kuna vitisho kwa hivyo ni onyo kwetu kulishughulika mapema kabla halijawa tatiza kubwa katika kanda ya maziwa makuu” alisema Mkuu wa Jeshi la Uganda, Jenerali David Muhoozi’

Kulingana na wakuu hao wa usalama kuna haja ya wao kushirikiana na majeshi ya mataifa ya kigeni yaliyochangia katika juhudi za kuvunja kundi hilo mashariki ya kati.

”Tishio la kundi hilo la kigaidi ni kubwa kiasi ya kuhamasisha Serikali za eneo hili lote la Maziwa Makuu, kuona ya kwamba zinaongeza juhudi za kukabiliana masuala ya kigaidi iwe ni kutoka kwa kundi la al-Shabab, ISIS, Boko Haram au Al-Qaeda”, alisema katibu mtendaji wa mataifa ya maziwa makuu, Zakaria Mubuli Mwita.

Aliongeza kuwa wamepokea ripoti kutoka kwa serikali za eneo hilo kwamba kundi la kigaidi la ADF linashirikiana na na makundi hayo ya kigaidi.

Hivi karibuni kundi la kigaidi la Islamic State lililo na chimbuko lake nchini Iraq, lilidai kufanya mashambulizi katika kijiji cha Kamango mkoani Kivu Kaskazini.

Maafisa wa kanda hiyo walisema hapakuwa na ushahidi wa IS kuhusika na shambulio hilo japo waliyoshuhudia walilaumu kundi la Allied Democratic Forces (ADF) ambalo wanadai limekuwa likishirikiana na IS.

Shambulio hilo la mwezi Aprili lilizua taharuki kuhusu hali ya usalama katika Mataifa ya Kanda ya Maziwa Makuu.

Bw. Zakaria Mwita ambaye ni Katibu Mkuu Mtendaji wa Mataifa ya Maziwa Makuu amesema kuwa wanapania kushirikiana na vikosi vya Umoja wa Mataifa kame vile MONUSC, Serikali na Jeshi la DRC pamoja na nchi zote za Maziwa Makuu ili kuona kuwa wanakabiliana vilivyo na makundi hayo ya kigaidi yasitie fora katika eneo hilo.

Ingawa maeneo karibu yote ya DRC yamekuwa yakikumbwa na changamoto za usalama kama vita ama kushambuliwa na waasi mara kwa mara, eneo la mashariki ya nchi hiyo ndiyo lililoathirika zaidi.

 

Usalama mashariki ya DRC

Akiongea na BBC siku chache kabla ya kuondoka madarakani mwishoni mwa maka 2018, rais mataafu wa nchi hiyo, Joseph Kabila alisema katika mambo ambayo angekuwa na muda zaidi kuyashughulikia ni kurudisha amani kwa taifa hilo.

Mashariki mwa DRC kuna makundi ya kijeshi ya waasi na ya kikabila.

Baadhi ya makundi yanaondwa na raia wa nchi hiyo, lakini kuna amakundi mengine makubwa ambayo yanafadhiliwa ama kupambana za serikali za nchi jirani.

Makundi ya waasi yanayotokea nchi jirani ni FDLR ambalo lilitekeleza mauaji ya kimbari nchini Rwanda mwaka 1994 na wapiganaji wake wakakimbilia DRC.

Waasi wa ADF wanatokea nchini Uganda.

Makundi hayo ya waasi yanatumia misitu mizito iliyopo kwenye eneo hilo kujificha na kuendesha shughuli zao huku wakitangaza nia ya kushambulia nchi zao walizozikimbia.

Uganda na Rwanda zimeshavamia DRC mara mbili kwa lengo la kusambaratisha makundi hayo na vita hizo kupelekea mamilioni ya watu kufariki.

 

 

 

cc;BBCswahili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *