KUWATAKA WATANZANIA KUCHANGIA STARS,KINANIFANYA NISHINDWE KUTAMBUA KAZI YA KAMATI YA USHINDI ILIYOUNDWA.

KUWATAKA WATANZANIA KUCHANGIA STARS,KINANIFANYA NISHINDWE KUTAMBUA KAZI YA KAMATI YA USHINDI ILIYOUNDWA.

Like
251
0
Monday, 02 November 2015
Slider

Na. Omary Katanga

Nianze kwa kuipongeza Tff kwa juhudi zake japo si madhubuti za kuiandaa timu yetu ya taifa, taifa stars katika harakati za kuiwania nafasi ya  kupangwa kwenye makundi ili kusaka tiketi ya kushiriki michuano ya kombe la dunia ifikapo mwaka 2018 huko nchini Urusi.

Nasema maandalizi siyo madhubuti nikilinganisha na yale yanayofanywa na mataifa mengine ambayo nayo yanaisaka nafasi hiyo kwa udi na uvumba,huku mashirikisho na serikali zao zikiwekeza kiasi kikubwa cha fedha kuhakikisha malengo yao yanatimia katika soka.

Hivi karibuni Stars imefanikiwa kuisukumiza nje Malawi katika patashika hizo,na hili bila kung’ata maneno jambo hilo limechangiwa na juhudi  za Tff na juhudi za watanzania likiwemo kundi maarufu la Stars Suporters waliojitoa kuiunga mkono kwa hali na mali timu yao popote iendapo.

Hivi karibuni  Tff imetangaza kamati iliyopewa jina la “Kamati ya Ushindi ya Stars” ambayo nayo imeunda vikamati vidogovidogo ikiwemo kamati ya uhamasishaji na masoko,zote hizi zikiwa na lengo la kile kinachoelezwa kuifanya stars ipate ushindi katika mechi dhidi ya Algeria inayokamata nafasi ya kwanza barani afrika katika viwango vya soka.

Lakini nimeshtuka kusikia  kamati hiyo imewataka watanzania kuichangia fedha kwa kile kinachodaiwa kuwa fedha hizo zitatumika kwa ajili ya motisha kwa wachezaji, uhamasishaji/masoko na maboresho ya kambi ya  stars ndani na nje ya nchi,kazi ambayo inapaswa kufanywa na mdhamnini kampuni ya bia TBL kupitia kinywaji chake cha Kilimanjaro.

Kwa mujibu wa mkataba kati ya Tff na TBL kuhusu udhamini wa Taifa Stars ,vitu kama maboresho ya Kambi,usafiri,posho za wachezaji ,vifaa nk.,vimo ndani yake ambavyo pamoja na mikakati mingine ya Tff na hamasa kwa watanzania ndivyo vilivyosaidia Stars kuitoa Malawi,kutoka sare dhidi ya Nigeria na Uganda pia.

Kwa hali ilivyo unaweza kujiuliza maswali mengi bila kupata majibu kwamba fedha hizo zinazokusanywa zinakwenda kufanya kazi gani wakati mdhamini anamaliza kila kitu?,hapa kamati inaweza kujikuta inapata lawama isizozozitarajia kuhusu zoezi hili.

Mara nyingi kamati kama hizi,zinajumuisha  wajumbe wenye uwezo wa kifedha,ambao watatumia uwezo wao kuboresha posho za wachezaji na benchi la ufundi,kuhamasisha na kuishauri Tff kuweka kiingilio kidogo kumuwezesha hata mtanzania wa hali ya chini kwenda kuishuhudia timu ya taifa lake.

Ikumbukwe kwamba watanzania hawa wanazo njia mbili tu za kuisaidia timu yao,ambazo ni kuishangilia kwa nguvu zote bila kujali itikadi za klabu zao,pamoja na kulipa kiingilio uwanjani kwa kutumia fedha zao wenyewe.

Tena utakubaliana na mimi kwamba Mara nyingi mashabiki wamekuwa wakipaza sauti zao kulalamikia kiasi kikubwa cha fedha kinachopangwa kama kiingilio cha kwenda kuiona timu yao,Kwa hiyo kitendo cha kuwataka waichangie kamati,ni kuwatwisha mzigo mzito.

Nionavyo mimi,Tff inapaswa kukaa na kitengo chake cha masoko na kuangalia njia sahihi itakayowezesha kupatikana kwa fedha ambazo zitaongeza nguvu kwenye zile zinazotolewa na mdhamini,kwa kuzungumza na makampuni na wafanyabiashara mbalimbali kwakuwa taifa stars hivi sasa inajitangaza kutokana na mwenendo ilionao.

Kwa kuwa timu ni yetu na nchi ni yetu,hakuna haja ya kuumizana kwa kuchangishana fedha,isipokuwa kila mmoja atimize wajibu wake,mashabiki walipe kiingilio na kwenda kushangilia kwa nguvu zote,Tff na mdhamini washughulikie maandalizi ya timu,Kamati ya ushindi ipambane kuzuia mbinu zozote chafu nje ya uwanja na kuweka mazingira ya kuwapumbaza wapinzani ili tanzania ipate ushindi.

Mwisho.

Comments are closed.