Mafuriko ya wasafiri, Wamiliki wa Mabasi waililia Serikali

Mafuriko ya wasafiri, Wamiliki wa Mabasi waililia Serikali

Like
1183
0
Tuesday, 11 December 2018
Local News

Kutokana na idadi kubwa ya abiria waliofurika katika vituo vya mabasi yaendayo mikoani kwa lengo la kusafiri katika msimu huu wa sikukuu za Christmas na Mwaka Mpya, wamiliki wa mabasi wameiomba Serikali kuzingatia ushauri wao ili kumudu hali iliyopo.

Katibu Mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi (TABOA), Enea Mrutu ameiomba Serikali kuruhusu mabasi ya abiria kusafiri usiku na mchana. Ameiomba Serikali kuongeza ulinzi kwa mabasi yanayotoka Dar es Salaam ili yasilale Shinyanga na badala yake yaruhusiwe kuingia Mwanza. Kadhalika, mabasi yanayotoka Mwanza kuelekea Dar es Salaam yasilale Morogoro kwa sababu ya usiku.

“Kwa mfano kutoka Shinyanga kwenda Mwanza kinachotakiwa pale ni kuongeza ‘patrol’ (doria) na kuhakikisha maeneo yote ya mizani kunakuwa na mtu wa kupima uzito wa magari na madereva wa mabasi na maroli kama wanatumia vilevi,” Mtanzania wanamkariri Mrutu.

Aidha, Mrutu aliitaka Serikali kuachana na mpango wake wa kusajili magari kwa ajili ya kuyaruhusu kusafirisha watu ili kuendana na mahitaji makubwa ya usafiri akieleza kuwa hatua hiyo inaweza kusababisha matatizo zaidi kwani madereva wa magari hayo hawana uzoefu na magari yao hayajafungiwa ving’amuzi vya kudhibiti mwendo (GPS).

Alisema badala yake Serikali ipunguze vizuizi na vituo ambavyo havina ulazima wa mabasi kuingia ikiwa hayana abiria ili kuokoa muda.

Katika hatua nyingine, Meneja wa Kituo Kikuu cha Mabasi cha Ubungo, Imani Kasagala amesema kuwa kuna viashiria kuwa mwaka huu kutakuwa na abiria wengi zaidi ya mwaka jana kwani katika theluthi ya kwanza ya kipindi hiki cha sikukuu tayari idadi imeanza kuwa kubwa, tofauti na mwaka jana ambapo idadi kubwa ilianza kuonekana katika theluthi ya pili.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *