Mahakama kutoa hukumu kesi ya Nguza Viking na mwanaye Papii Kocha Tanzania

Mahakama kutoa hukumu kesi ya Nguza Viking na mwanaye Papii Kocha Tanzania

Like
658
0
Friday, 23 March 2018
Local News

 

Mahakama ya Afrika na Haki za Binadamu (AfCHPR) inatoa hukumu katika kesi iliyowasilishwa na wanamuziki Nguza Viking maarufu Babu Seya na mwanaye, Johnson Nguza ‘Papii Kocha’ dhidi ya serikali ya Tanzania katika mahakama hiyo.

Wawili hao waliwasilisha rufaa katika mahakama hiyo mwaka 2015 kupinga hukumu ya kifungo cha maisha iliyokuwa imetolewa dhidi yao.
Walikuwa wanatumikia kifungo cha maisha jela kwa kuwabaka wasichana 10 wa shule waliokuwa na kati ya umri wa miaka 6 na 8 mwaka 2003.
Walikuwa wametumikia kifungo cha miaka 13 kufikia wakati wa kupewa msamaha
Babu Seya ambaye ni miongoni mwa wafungwa 1,821 waliosamehewa na Rais John Magufuli siku ya Uhuru wa Tanganyika mnamo 9 Desemba, 2017.
Wengine 8157 walipunguziwa adhabu zao.
Wawili hao ndio walioimba kibao maarufu cha ‘Seya’ na walikuwa kati ya wafungwa 61 waliokuwa wamehukumiwa kufungwa maisha au kunyonga ambao walinufaika kutokana na msamaha wa rais.
Wafungwa waliosamehewa wamshukuru Magufuli kwa kumwimbia
Babu Seya na wanawe waachiwa huru kwa msamaha wa rais
Hukumu katika kesi yao ilikuwa imepangiwa kusomwa Jumatano wiki hii lakini baadaye ikaahirishwa hadi leo.

Hatua ya Dkt Magufuli kuwasamehea wawili hao ilishutumiwa na watetezi wa haki za watoto na wanawake.
Kate McAlpine, mkurugenzi wa shirika la Community for Children Rights lenye makao yake Arusha aliambia BBC wakati huo kwamba alikuwa “ameshtushwa lakini hakushangazwa” na hatua ya rais huyo. Alisema hatua hiyo ilionesha ‘uelewa mdogo’ wa kiongozi huyo kuhusu masuala ya udhalilishaji wa watoto.

Alilinganisha hatua hiyo na tamko la Rais Magufuli kwamba wasichana wanaoshika mimba hawafai kuwa shuleni.
Matamshi ya Magufuli yawakasirisha wanawake Tanzania
“Huwa hafahamu vyema mambo, hasa yanayohusu watoto kama waathiriwa. Wasichana wanaoenda shule hushika mimba kwa sababu mara nyingi ni waathiriwa wa udhalilishaji,” alisema Bi McAlpine.
Wakishinda watadai fidia?
Kwa kuwa wawili hao walishasamehewa na rais, uwezekano wao kuchukuliwa hatua iwapo hukumu ya kifungo dhidi yao itadumishwa ni mdogo sana.
Hata hivyo, iwapo watapatikana bila hatia, kuna uwezekano huenda wakawasilisha kesi wakitaka walipwe fidia kwa kipindi ambacho walikaa gerezani.
Ilikuwaje hadi tukafika hapa?
Nguza Viking na Johnson Nguza ni baba na mwanaye na ni raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambao walikuwa wanamuziki Dar es Salaam.
Wote walikamatwa 12 Oktoba, 2003 na kuzuiliwa kituo cha polisi cha Magomeni ambapo baadaye walifikishwa kizimbani Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu 16 Oktoba, 2003 na kufunguliwa mashtaka 10 ya ubakaji na 11 ya ulawiti.
Waathiriwa wao walikuwa watoto wa kati ya miaka sita na nane, na walikuwa wote kutoka darasa moja.
Waathiriwa hao walidaiwa kubakwa na kulawitiwa kwa zamu na wanaume watano.
Mnamo 25 Juni, 2004 hakimu aliwapata na hatia na kuwafunga jela Nguza na wanawe watatu. Mshtakiwa wa nne, ambaye alikuwa mwalimu, alipatikana bila hatia.
Washtakiwa walikata rufaa Mahakama Kuu lakini rufaa yao ikatupwa.
Walikata rufaa tena katika Mahakama ya Rufaa.
Wawili kupatikana bila hatia
Mwaka 2010 rufaa yao ilisikilizwa na 30 Oktoba Majaji Nathalia Kimaro, akisaidiana na Mbarouk Mbarouk na Salum Masati katika Mahakama ya Rufaa wakawaachilia huru Nguza Mashine na Francis Nguza baada ya kuwapata bila hatia.
Babu Seya na mwanaye Papii Kocha walipatikana na hatia na hivyo kuendelea kutumikia adhabu ya kifungo cha maisha jela.
Majaji walisema kuwa kuna uthibitisho kuwa warufani hao wawili waliwabaka watoto wa shule ya msingi mwaka 2003.
Kesi hiyo iliwashtua mashabiki wa mwanamuziki Viking nchini Tanzania, na kanda nzima ya Afrika Mashariki.
Mwanamuziki huyo mwenye kuimba nyimbo za rhumba, ambaye ni mzaliwa wa DRC, ameishi Tanzania kwa miaka mingi na kuwa na mashabiki wengi.

 

Comments are closed.