MAHAKIMU 11 KIBARUA CHAOTA NYASI

MAHAKIMU 11 KIBARUA CHAOTA NYASI

Like
249
0
Thursday, 08 September 2016
Slider

Dar es Salaam. Wakati mahakimu 11 na watumishi 23 wa mahakama wakifukuzwa kutokana na kukiuka maadili ya utumishi, wengine 62 watajadiliwa na vyombo vya kimahakama kuangalia hatima yao.

Akizungumza baada ya kupokea ripoti ya miezi minane ya utendaji wa mahakama Jaji Mkuu Mohamed Chande Othman amesema mahakimu 32 walioshinda kesi za jinai katika mahakama mbalimbali nchini, watapelekwa kwenye Kamati ya Maadili ya Mahakama kwa ajili ya kufunguliwa mashauri ya kinidhamu.

Amesema mahakimu wengine 30 walioshinda kesi za rushwa katika mahakama mbalimbali watapelekwa kwenye Tume ya Mahakama kwa ajili ya kujadiliwa na kuangalia hatima yao. “Wakati mwingine Mahakama inaweza isione tatizo lao, lakini kiutendaji lazima tujiridhishe, tuangalie mambo yaliyokuwamo katika kesi zilizokuwa zinawakabili na kuchukua hatua za kimaadili,” amesema Jaji Chande.

Hata hivyo, amesema pamoja na kuwa idadi hiyo ni ndogo kati ya watendaji 6,406, hilo ni doa kubwa kwa mhimili huo wa dola. “Ni idadi ndogo ni sawa na asilimia 0.005 lakini kwa mahakama ni doa na haiwezi kuvumilika,” amesema Chande.

Jaji Chande alitaja baadhi ya makosa waliyokutwa nayo baadhi ya mahakimu hao kuwa ni kutumia muhuri wa mahakama kwa manufaa binafsi, kumsaidia mtu kufungua kesi katika mahakama mbili tofauti na mwingine kufungua shauri la mirathi bila kuwa na hati ya kifo. Amesema kuna makosa ya kisheria yasiyowajibishwa na yanayowajibishwa yakiwamo hayo ya kufanya mzaha wa kisheria.

Comments are closed.