Millicent Kagonga, ameugua saratani ya mlango wa uzazi kwa miaka 9, na anasema maisha yake hayajakuwa rahisi.
Saratani ya mlango wa uzazi inaweza kusababishwa kwa maambukizi ya virusi vya Human Papillomavirus au HPV, na aina hii ya virusi huambukizwa kwa njia ya kujamiiana.
Alianza kuhisi kwamba ana tatizo alipojifungua mtoto wake wa tatu akiwa na miaka 20, ambapo alianza kutokwa na uchafu katika sehemu za siri lakini hakujua ulikuwa ni ugonjwa gani.
“Baada ya muda nikaanza kuvuja damu na hapo nilikwenda hospitalini na daktari akasema ”Dada pole unaugua satarani na iko katika kiwango cha nne.”
”Nilipoteza fahamu na hata wakati huo nilitaka kujitoa uhai na hata watoto wangu wawili kwa sababu ya maisha niliyoyapitia, singependa mtoto wangu apitie hayo”.
Bi, Milicent anazungumza akiwa amelala kwenye sakafu kwani hawezi kuketi kwa muda mrefu kutokana na shida ya mgongo na hata kusumbuliwa na misuli.
”Wakati nilipokuwa nimekaa na saratani hiyo kwa muda sikuweza kuzuia haja ndogo au kubwa, nilikuwa navuja damu mara mbili kwa siku kwa dakika tano na nilikuwa nikipoteza zaidi ya lita nne za damu asubuhi na nne jioni”.
”Lakini siwezi kusahau ile siku nilivuja damu kwa siku mbili”.
‘Nilitokwa na uchafu ulionuka kutoka sehemu zangu za siri kwa miaka sita, kwa sababu sikujua naugua ugonjwa gani? Nilivumilia kwa sababu niliogopa kubaguliwa na ndoa yangu kuvunjika,”Millicent anasema.
Kwa kupitia matibabu haya ya saratani Millicent anasema kwa hivi sasa hawezi kukaa kwenye kiti kwa muda mrefu au hata kulala kitandani. Iliyobaki analala sakafuni kwa sababu ya maumivu makali mgongoni mwake.
Millicent ameongeza kwamba alifika ukomo wa uzazi wa mapema, na hata kuwa mnene kutokana na matibabu hayo.
Safari yake ya ugonjwa huo haikukomea hapo, alianza kutengwa akabaki na watoto wake pekee, na hakuna mtu aliyetaka kujihusishwa naye.
Jamii yake ilisema kwamba amerogwa, wenine wakasema ni kiboko anachochapwa kutoka kwa maulana na hata wengine wakisema ni laana ya kuzaliwa nayo, kwa jinsi alivyokuwa akivuja damu.
”Kama si matibabu ya kuchomwa na miale ya moto, basi leo hii singekuwa hai,” Millicent anasema.
Saratani hii haina dalili hadi inapofika kiwango kikuu. Mara nyingi wanawake hudhani dalili wanazopata ni za kitu kingine, kama vile hedhi ya kila mwezi, maambukizi katika kibofu cha mkojo, au kuvu.
Kwa mujibu wa shirika la afya duniani, WHO, hizi ndizo baadhi ya dalili zinazojitokeza kwa muathiriwa:
Ni muhimu kwa wanawake wote kufanyiwa ukaguzi wa fuko, au mlango wa uzazi na kupata ushauri wa daktari iwapo baadhi ya dalili zitajitokeza.
Kuna saabu nyingi za kukufanya ukavuja damu kupita kiasi na huenda sio saratani ya mlango wa uzazi. Na mambo mengi huzingatiwa katika kulibaini hilo, mfano umri, uzazi, iwapo umejifungua na pia historia ya familia.
Kadhalika kuvuja damu baada ya ukomo wa uzazi ni jambo la kawaida, hatahivyo ni vyema kupata ushauri wa daktari wako.