Na.Omary Katanga
Ligi kuu msimu wa 2014/15 imemalizika kwa style ya aina yake,malalamiko ya waamuzi kuvibeba baadhi ya vilabu,miundombinu mibovu katika baadhi ya viwanja,adhabu lukuki toka kamati ya usimamizi wa ligi kwenda kwa vilabu na makocha,vimechukua nafasi kubwa.
Jambo baya zaidi kutokea msimu huu ambalo halipaswi kuchelewesha utatuzi wake,ni madai ya kuwepo na upulizwaji wa dawa za kunyong’onyesha viungo vya wachezaji katika vyumba vya kubadilishia nguo kwenye uwanja wa Kambarage huko Shinyanga,kitendo kinachodaiwa kufanywa muda mfupi kabla ya mpira kuanza.
Hali hii imeviogopesha vilabu karibu vyote vilivyocheza katika uwanja huo na kugoma kuingia vyumbani kukwepa madhara ,lakini kwa mujibu wa kanuni inayosimamiwa na bodi ya ligi,vilabu hivyo vimepigwa faini kwa kukiuka kanuni.
Swali la kujiuliza,kwanini uwanja wa Kambarage ndio unaonyooshewa kidole na walio wengi? Hapa utagundua kuwa tatizo hilo lipo na linapaswa kushughulikiwa kwa haraka na TFF ambao ndio wasimamizi wakuu wa mpira nchini.
Jamal Emil Malinzi,ni rais wa TFF,ambaye anayo mamlaka makubwa ya kuondoa kero hizi kupitia kamati zake mbalimbali alizoziunda kwa utashi wake,lakini chakushangaza kumekuwa na hali ya kusuasua katika utekelezaji wake,na badala yake mkazo zaidi umewekwa kwenye kuvipiga faini vilabu,makocha na wachezaji.
Hivi karibuni amepandishwa ndege mkurugenzi wa mashindano wa TFF,Boniface Wambura, na baadaye akafuatiwa na afisa wa Ligi, Joel Balisidya, kwenda Shinyanga kujionea hali ilivyo lakini tangu wamerudi taarifa zao zimefungiwa kabatini, kitendo kinachotafsiriwa kuwa ni upuuzwaji mkubwa wa malalamiko ya vilabu.
Wapi vilabu vikimbilie kupata haki zao za msingi kama si kwa mamlaka inayohusika (TFF),lakini kama kelele zao zinaonekana hazina maana,basi wanaofanya vitendo vya upulizaji dawa mbaya ya kuangamiza wachezaji na waendelee na kazi yao ,lakini Malinzi ni lazima utambue kwamba ipo siku watanzania watakuhukumu kwa kuyazibia masikio malalamiko yao.
Nakushauri Malinzi,ondoa Pamba masikioni mwako usikilize na kuyashughulikia malalamiko ya vilabu ili kukomesha uozo unaoendelea katika ligi ya nchini hii,kwa kushindwa kufanya hivyo jamii ya watu wa mpira na watanzania kwa ujumla,hawatakuelewa.
Mwisho.