MALINZI USIONE HAYA KUMPA “MAKAVU” KOCHA STARS

MALINZI USIONE HAYA KUMPA “MAKAVU” KOCHA STARS

Like
299
0
Monday, 25 May 2015
Slider

 

Na Omary Katanga.

Ni jambo la kuhuzunisha kuona timu yetu ya taifa Taifa Stars,ikigeuzwa kama pombe ya ngomani kila mmoja anajinywea atakavyo,huku maneno ya kutia moyo kutoka kwa viongozi wa shirikisho la mpira nchini TFF yakiendelea kushika hatamu.

Tangu mwanzoni uamuzi wa rais wa TFF,Jamali Malinzi wa kuvunja mkataba wa kocha Kim Polsen (Denmark) na kukubali kulipa mamilioni ya shilingi kama fidia ili aondoke na kumleta kocha wa sasa Martin Nooij (Uholanzi),ulipokelewa kwa shingo upande na wadau wa soka.

Uamuzi huu ulitafsiriwa kama ubabe wa madaraka,wakati ambapo wadau wakihoji  mshahara mkubwa anaolipwa kocha usiolingana na kazi yake,lakini Malinzi hakutilia maanani madai hayo na kuamua kutafuta fedha kwa njia anazozijua yeye ili mradi kutimiza lengo lake.

Ni ukweli usiopingika kocha Nooij hana uwezo wa kuifanya Stars kuwa na mafanikio wanayoyahitaji watanzania,kwani tangu ajiunge nayo amefanikiwa kupata ushindi katika mechi tatu,kwenda sare mechi tano na kufungwa mechi saba zikiwemo za kirafiki,kufuzu AFCON na Michuano ya COSAFA.

Matokeo haya mabovu yanazidi kuondoa matumaini ya watanzania kuona kama ipo siku wataifurahia timu yao,na hivyo kupelekea idadi ya watazamaji kupungua uwanjani kila Stars inapocheza,na wachache kati yao wanakwenda uwanjani kwa lengo la kuangalia wachezaji wa vilabu vyao tu.

Nina mashaka makubwa na washauri wa karibu wa rais Malinzi linapokuja suala la timu ya taifa,miongoni mwao hujifanya wanajua zaidi kiasi cha kudiriki hata kuingilia kazi ya benchi la ufundi kwa kumchagulia kocha wachezaji.

Na hili limejidhihirisha pale kocha alipotangaza kikosi chake kwaajili ya michuano ya COSAFA kikiwa na wachezaji ambao hata kwenye vilabu vyao hawajacheza kwa kipindi kirefu ,na kuibua maswali kwa  wadau wa soka wakihoji-ni wapi Kocha Nooij ameona uwezo wao?

Wakati umefika sasa wa kuambiana ukweli juu ya hali mbaya iliyonayo Stars,lakini ukweli huo unaweza kugeuzwa kama ni mapambano na uongozi uliopo madarakani,ambao baadhi yao hawapendi kuonekana wameshindwa kutimiza wajibu wao.

Kwa hali hii naishauri TFF kuchukua maamuzi magumu ya kusafisha benchi karibu lote la ufundi na kuangalia mbadala wake, kwa kuwashirikisha makocha wa zamani na wadau wengine wa mpira,ili kuleta mabadiliko kwenye kikosi cha taifa kinachojiandaa na michuano ya kufuzu AFCON, 2017.

mwisho.

 

 

 

Comments are closed.