Mamia watumia njia ya mkato katika mbio za Marathon, China

Mamia watumia njia ya mkato katika mbio za Marathon, China

1
619
0
Friday, 30 November 2018
Global News

Wanariadha takriban 250 waliokuwa wanashiriki mbio za half marathon nchini China walinaswa na kamera za siri wakitumia njia ya mkato kumaliza mbio hizo.

Wengi walipitia vichakani na wengine kwenye vichochoro.

Waandalizi wa mbio hizo zilizofanyika Shenzhen, China, wanasema waligundua pia wakimbiaji 18 waliokuwa wamevalia vibango vya nambari za kuwatambua wanariadha vilivyokuwa bandia.

Kulikuwa pia na wanariadha watatu ambao wameelezwa kuwa wanariadha walaghai waliokuwa wanajifanya kuwa watu tofauti.

Wote waliopatikana wakifanya udanganyifu huo sasa wanakabiliwa na uwezekano wa kupigwa marufuku.

“Marathon si jambo rahisi tu eti la kufanya mazoezi, ni tuseme kama mfano wa maisha yalivyo, kila mkimbiaji anajiwajibikia mwenyewe,” waandalizi walisema.

Video za kamera za polisi watrafiki zinawaonesha wakimbiaji hao wakitokomea kwenye vichaka vilivyo karibu na barabara kuu iliyokuwa inatumiwa badala ya kuendelea na barabara hiyo kisha kujipinda ilivyo barabara hiyo.

Waandalizi wanasema watu hao 237 waliopatikana wakidanganya kuna uwezekano walipunguza umbali wa kukimbia mbio hizo za kilomita 21 kwa kilomita mbili au tatu hivi.

Mbio za Shenzhen Half Marathon ambazo hufanyika kila mwaka katika jiji hilo la nne kwa wingi wa watu China kwa wastani huwavutia washiriki 16,000.

Taarifa za udanganyivu huo zililifanya gazeti la People’s Daily la China – moja ya magazeti yanayosomwa zaidi China – kuwahimiza wakimbiaji “kuheshimu mbio hizo za marathon na kuheshimu moyo wa michezo pia” kwenye tahariri yake.

Mwaka jana, waandalizi wa Beijing Half Marathon walianza kutumia mfumo wa kuwatambua watu kwa nyuso zao kuzuia wanariadha kuwatumia watu wengine kukimbia kwa niaba yao.

China imeandaa mashindano 1,072 ya marathon na mbio nyingine za nyika mwaka huu, idadi hii ikiwa imeongezeka kutoka 22 mwaka 22, kwa mujibu wa Chama cha Riadha cha China.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *