Mapigano yamezuka tena nchini Sudan Kusini saa chache baada ya Umoja wa Mataifa kuhimiza pande hasimu kusitisha vita.
Mwanahabari aliyeko mjini Juba ameambia BBC kwamba milio ya risasi na milipuko mikubwa imeanza kusikika kote mjini humo.
Amesema silaha nzito zinatumika kwenye vita hivyo.
Mapigano yamekuwa yakiendelea kwa siku kadha kati ya wanajeshi watiifu kwa Rais Salva Kiir na wanajeshi watiifu kwa Makamu wa Rais Dkt Riek Machar.
Vituo vya Umoja wa Mataifa pamoja na maeneo ya raia pia yameshambuliwa, jambo ambalo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linasema huenda likawa uhalifu wa kivita.
Mapigano hayo yamesababisha mashirika ya ndege kusitisha safari za kuingia na kutoka Juba.
Serikali za mataifa mengi ya kigeni zimewahimiza raia wake kuchukua tahadhari. Baadhi, zimeanza kuchukua hatua kuwaondoa maafisa wake nchini humo.
Canada imetangaza kufunga ubalozi wake na ikawashauri raia wake kutozuru taifa hilo ambalo liliadhimisha miaka mitano tangu kujipatia uhuru Jumamosi.
Viongozi wa mataifa ya kanda ya Afrika Mashariki wametoa wito wa kusitishwa kwa mapigano.
Mawaziri wa nchi wanachama wa IGAD wanakutana leo alasiri jijini Nairobi kujadili hali nchini Sudan Kusini.
Wanajeshi wawili wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Uchina wamefariki baada ya kushambuliwa.