Marais 27 wa bara la Afrika Jumatano wamesaini makubaliano ya kuanzisha soko huria barani Afrika huko nchini Rwanda.
Pia marais hao wamepongeza uamuzi huo na kusema kuwa hiyo ni hatua ya mwanzo kabisa ya kuleta mapinduzi ya kujikwamua kiuchumi katika bara hilo.
Rais wa Rwanda Paul Kagame ambaye pia ni mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU) amesema kwamba ufanisi wa makubaliano haya utategemea zaidi utekelezaji wa mikataba ya umoja wa kanda ambayo imekuwepo kwenye bara hilo kwa miaka mingi sasa.
Kagame ameongeza kuwa kutekelezwa kwa makubaliano haya kutategemea pia mabadiliko yanayoendelea kufanyika kwenye kanda hizo za kiuchumi barani Afrika ili kuwepo uhuru na wepesi wa kuyetekeleza
Viongozi waliozungumza wamesema kwamba siku ya leo ni muhimu kwa sababu ni mara ya kwanza kutekelezwa kwa ndoto ya viongozi wa kiafrika waliotangalia ambao walikuwa wanataka kuliona bara la Afrika siku moja limeungana na wakazi wake wakitembea bila vipingamizi.
Kwa mantiki hii wengi wamesema kwamba hatua hii si kusaini tu makubaliano haya lakini ni hatua muhimu ya kuthubutu kutekeleza mkakati mpana wa kufikia ile hatua kubwa ya kuifikia ‘’Afrika tuitakayo’’.
Hata hivyo makubaliano haya yanasainiwa huku Nigeria ambayo ni taifa kubwa la kiuchumi kwa sasa barani Afrika likiwa halikusaini na kuomba wapewe muda wa kutathmini suala hilo.