MAWAKALA ONGOZENI WACHEZAJI KUSOMA MIKATABA KABLA YA KUISAINI.

MAWAKALA ONGOZENI WACHEZAJI KUSOMA MIKATABA KABLA YA KUISAINI.

Like
274
0
Monday, 14 December 2015
Slider
Na. Omary Katanga………………………………..+255784500028
Kila unapofika wakati wa usajili kwa wachezaji kutoka klabu moja kwenda kujiunga na klabu nyingine,malalamiko,vitisho,ubabe na hata kutunishiana misuli kwa baadhi ya viongozi wa klabu kwa kile kinachoonekana wengine kufuata kanuni na wengine kuzitupilia mbali.
Tofauti na Tanzania,kwa upande wa nchi nyingine zilizoendelea kisoka duniani huwezi kusikia malalamiko kama hayo yaliyopo hapa nchini kuhusu usajili,na hii ni kutokana na utaratibu mzuri uliokuwepo kati ya mawakala,wachezaji na klabu zenyewe.
Karibu asilimia 95 ya wachezaji hapa nchini hawana watu wanaowasimamia katika masuala mbalimbali ya kimikataba,endapo mchezaji atahitaji kuhama klabu moja kwenda nyingine,au kuvuka mipaka kwenda nje ya nchi kucheza soka la kulipwa,tofauti na ilivyo kwa nchi nyingine.
Kama inavyofahamika duniani kote,mchezo wa soka ni moja ya ajira iliyo rasmi ambapo vijana wengi wamekuwa wakijitumbukiza huko ingawa wengi wao wameshindwa kabisa kupata mafanikio, kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kukosa muongozo sahihi katika ajira yake hiyo ya kusakata kandanda.
Hali hiyo inapelekea wadau mbalimbali wa soka kupeleka lawama zao kwa klabu bila ya kujua chimbuko la kutofanikiwa kwa mchezaji husika ni nini,na hapo vurugu ndipo zinapoibuka hadi kusababisha mchezaji wakati mwingine kujikuta akishindwa kabisa kucheza mpira na kuanza kuhangaika mtaani.
Nimekuwa nikizungumza mara kwa mara na uongozi wa chama cha wacheza soka nchini SPUTANZA,chini ya mwenyekiti wake Musa Kisoki,kuhusu madhumuni ya kukianzisha chama hicho,naye akanieleza kuwa ni kutetea na kulinda maslahi ya wachezaji,lakini ninachokishuhudia ni vurugu tupu kati ya uongozi wa klabu,Tff na SPUTANZA wenyewe.
Uchunguzi nilioufanya nimebaini kuwa vurugu hizo zinasababishwa na uswahiba uliopo kati ya viongozi wa klabu na Tff,ambapo licha ya kuwepo na kanuni za usajili zinazoonesha pia adhabu inayoweza kutolewa kwa klabu inayokiuka kanuni hizo,lakini bado uvunjaji huo unaendelea kufanywa tena mchana kweupe.
Uswahiba huo unasababisha pia baadhi ya klabu kuchezea kwa kubadilisha vipengele vilivyomo katika mikataba elekezi ya usajili inayotolewa na Tff,kwa lengo la kujinufaisha wao na kumkandamiza mchezaji,kwa kuwa tu hana mtu mwenye ufahamu wa kutosha wa kuisoma na kuielewa mikataba.
Nitumie nafasi hii kuwakumbusha wachezaji wote wanaojitambua na wasiojitambua,kuhakikisha anakuwa na mtu wa kumuongoza na kumsimamia katika zoezi zima la kuingia mikataba,ili kulinda utu na maslahi yake kwa kipindi chote anapokuwa katika ajira yake ya kucheza mpira.
Wakati mwingine mchezaji anaweza kujiongeza mwenyewe wakati anapotaka kuingia mkataba na klabu,asiweweseke na rundo la pesa anazowekewa mezani ili kumshawishi kuweka saini kwenye mkataba ambao huenda unavipengele vitakavyomletea usumbufu mbele ya safari.
Lakini kwa upande wa Tff,wakati wa uswahiba sasa umepitwa na wakati na muhakikishe kanuni na taratibu zote za usajili mlizoziweka nyinyi wenyewe zinatekelezwa kwa usahihi bila ya kupendelea wala kukandamiza upande wowote,kama kweli mmedhamiria kwa dhati kusimamia soka la nchi hii.
Nimalizie kwa kuzitakia mafanikio mazuri klabu zote zinazoshuka dimbani leo katika patashika za ligi kuu Tanzania bara inayorejea baada ya mapumziko ya takribani mwezi mmoja.
MWISHO.

Comments are closed.