Mchezaji wa QPR Adel Taarabt amemjibu kocha wake Harry Redknapp aliyesema kuwa mchezaji huyo ana uzani mkubwa hivyobasi hafai kucheza.
Redknapp alitoa madai hayo alipoulizwa ni kwa nini hakumjumuisha kiungo huyo wa kati katika kikosi kilichocheza mechi dhidi ya Liverpool waliposhindwa kwa mabao 3-2. Hata hivyo Taarabt alipokuwa akiongea na kituo cha habari cha Daily Mail alijitetea kwamba madai hayo si ya kweli.
“Nilikuwa na tamaa kubwa ya kucheza kabla ya mechi kuanza. Nilikasirika sana niliponyimwa nafasi ya kucheza.”alisema Taarabt.
Taarabt, ambaye hajakuwa akishirikishwa katika vipindi vya kwanza vya mechi za QPR tangu Agosti 27 alisema: “Mwanahabari alikuwa akifanya wajibu wake kwa kuuliza kama nilikuwa na jeraha”. ” Angesema ”atakapokuwa sawa atacheza”. Yeye ni meneja mwenye tajriba kubwa na angedhibiti hali ilivyokuwa”
“Sikushiriki mechi za kabla ya msimu kuanza kwa sababu nilikuwa na jeraha la kisigino, kwa hivyo hali yangu haikuwa asilimia mia kwa mia.”
Taarabt alirudi kuichezea Loftus Road msimu huu baada ya kuzichezea Fulham na AC Milan msimu uliopita kwa mkopo.
” Sipendi chakula tunachopewa katika kambi ya kufanyia mazoezi lakini nala chakula bora kama wachezaji wengine.
“Uzani mkubwa ambao nimewahi kuwa nao ni kilo 86 nikiwa AC Milan, uzani mdogo Zaidi ukiwa kilo 84 na kwa sasa nina uzani wa kilo 85.”
Timu ya QPR inashika mkia katika orodha ya ubora wa timu katika ligi ya Uingereza baada ya kujipatia pointi nne tu katika mechi nane za mwanzo wa msimu huu walizoshiriki.