MFUMUKO WA BEI

MFUMUKO WA BEI

1
488
0
Wednesday, 02 May 2018
Local News

 

Dar es Salaam. Watumiaji magari, mashine na mitambo inayotumia petroli na dizeli watapata ahueni baada ya bei ya bidhaa hizo kupungua, huku bei ya mafuta ya taa ikipanda.
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), jana ilitangaza kushuka kwa bei ya petroli na dizeli kwa asilimia 2.7 na asilimia 3.8; na ongezeko la asilimia 0.09 kwa mafuta ya taa.
Taarifa iliyotolewa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Nzingagwa Mchany ilisema bei hizo mpya zitatumika Tanzania Bara kuanzia leo.
Hata hivyo, kwa watumiaji wa mafuta yanayopitia katika Bandari ya Dar es Salaam ni neema, lakini wa Bandari ya Tanga bei imeongezeka.
Mchany alisema mabadiliko hayo ya yanatokana na kushuka kwa bei ya mafuta katika soko la dunia na marekebisho ya bei yaliyofanywa na Ewura kutokana na kubadilika kwa tozo za wakala na Serikali za mitaa katika bidhaa hizo.
Ikilinganishwa na tangazo la bei ya mafuta la Aprili 4 kwa mafuta yanayopitia katika Bandari ya Dar es Salaam, bei ya petroli imepungua kwa Sh88 kwa lita (asilimia 3.8) na dizeli Sh61 kwa lita (asilimia 2.75); huku bei ya mafuta ya taa ikiongezeka kwa Sh2 kwa lita sawa na asilimia 0.09.
Tofauti na wanunuzi wa rejareja, bei ya wale wa jumla upande wa petroli imepungua kwa Sh100.91 kwa lita (asilimia 4.58), dizeli Sh73.71 kwa lita (asilimia 3.52) na mafuta ya taa Sh10.49 kwa lita sawa na asilimia 0.51.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *