MICHUANO YA AFRIKA CONGO BRAZAVILE ,TANZANIA NI NDOTO KUPATA MEDALI KWENYE MASUMBWI

MICHUANO YA AFRIKA CONGO BRAZAVILE ,TANZANIA NI NDOTO KUPATA MEDALI KWENYE MASUMBWI

Like
299
0
Monday, 31 August 2015
Slider

Na Omary Katanga

Michuano ya afrika maarufu kama All African Games,inafunguliwa rasmi septemba 4 mwaka huu katika uwanja wa New Kintele nchini Congo Brazavile ,kwa mataifa yote 54 ya afrika kushiriki katika mashindano hayo.

Tanzania ni miongoni mwa mataifa hayo ambayo itapeleka timu za michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu,Riadha,Judo,Masumbwi na mingine mingi,lakini kwa hali jinsi ilivyo hakuna uhakika hata kidogo wa kuambulia medali ya aina yeyote kutokana na idadi ndogo ya wachezaji waliopangwa kushiriki mashindano hayo mwaka huu.

Hebu tuiangalie timu ya masumbwi ambayo nayo ipo kambini kujiandaa na mashindano hayo ikiwa na jumla ya mabondia 17,ambao wanasubiri mchujo wa mwisho wa kocha wa timu hiyo ya taifa ili kupata mabondia watakaosafiri kwenda Congo.

Taarifa ya serikali kuhusu idadi ndogo ya mabondia watakaopata nafasi ya kwenda kwenye mashindano hayo,ndiyo iliyonifanya nifunguke kuandika haya kwa uchungu mkubwa,baada ya kuona juhudi za kujitoa za mabondia hao 17 walio kambini kujipanga kulitetea taifa zikiyeyuka.

Nilizungumza na katibu mkuu wa shirikisho la masumbwi ya ridhaa nchini BFT,Makore Mashaga,akanieleza kuwa wamepokea taarifa kutoka serikalini kwamba idadi ya mabondia watakaokuwemo kwenye safari ya kushiriki mashindano hayo makubwa barani afrika ni watatu tu,kati ya wale 17 wanaofanya mazoezi,kutokana uhaba wa fedha za kusafirisha idadi kubwa ya mabondia.

Idadi hiyo imezidi kupungua ikilinganishwa na ile ya walioshiriki  mashindano ya jumuiya ya madola yaliyofanyika mwezi julai mwaka uliopita huko katika mji wa Glasgow nchini Scotland,ambapo mabondia waliofanikiwa kwenda huko walikuwa wa tano,idadi ambayo hata hivyo ilikuwa ndogo kulinganisha na mataifa mengine waliopeleka mabondia zaidi ya 10.

 

Hata hivyo safari ya mabondia hao watano ilikuwa ya shingo upande baada kuwepo pia na malalamiko ya posho za kujikimu wakiwa ugenini,hali iliyopelekea kushindwa kabisa kufurukuta mbele ya mataifa mengine.

Hebu tuyaache hayo yaliyopita, na tuelekeze macho na masikio yetu kwenye uwanja wa New Kintele huko Congo Brazavile,ambapo mbali na timu ya masumbwi kuwa na idadi ndogo ya mabondia,timu nyingine ni ile ya Judo ambayo wao wameruhusiwa kupeleka wachezaji wawili tu.

Nilizungumza na kiongozi mmoja wa chama cha Judo kutaka kujua sababu ya kupeleka wachezaji hao wawili ,lakini jibu lake halikutofautiana na la upande wa masumbwi kwamba serikali imesema haina uwezo wa kugharamia wachezaji wengi kwenda kwenye mashindano hayo.

Kwa hali hii pekee inatosha kusema kuwa ni ndoto kwa tanzania kupata hata medali ya bati katika mashindano hayo,lakini hata hivyo nizitakie kila la kheri na maandalizi mema timu zote zitakazoshiriki mashindano hayo.

Mwisho.

Comments are closed.