Wakili na mwanaharakati mzaliwa wa Kenya ambaye alilazimishwa kwenda uhamishoni nchini Canada mwezi Februari mwaka huu alitarajiwa kurejea mjini Nairobi siku ya Jumatatu Machi 26, 2018 huku kukiwa na wasiwasi kwamba huenda asiruhusiwe na serikali ya Kenya kuingia nchini.
Katika taarifa aliyoituma kwa idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Amerika siku ya Jumapili akiwa mjini London Uingereza, Miguna Miguna alisema kuwa ataingia Kenya hata bila pasipoti au viza kumruhusu kufanya hivyo.
“Ndege yetu itatua Nairobi Jumatatu saa nane na dakika kumi na tano alasiri,” alisema Miguna.
Wakati wa kuchapisha ripoti hii, serikali ya Kenya haikuwa imetekeleza maagizo ya mahakama kuu, kuitaka imrejeshee hati yake ya kusafiria.
Miguna, ambaye amejitangaza kuwa kiongozi wa vuguvugu la National Resistance Movement (NRM- Kenya), amekuwa akiishi uhamishoni tangu maafisa wa polisi walipomlazimisha kuabiri ndege katika uwanja wa kimataifa wa Jomo Kenyatta mjini Nairobi mapema mwezi Februari, kwa madai kwamba yeye si raia wa Kenya.
Mapema mwezi Februari, serikali ya Kenya iliwasilisha hoja mahakamani na kudai kuwa Miguna aliukana rasmi uraia wake na kwa hivyo hastaili kudai kuwa Mkenya.
Lakini mwanasiasa huyo mwenye utata ameshikilia kwamba katiba ya Kenya inaeleza bayana kuwa mtu aliyezaliwa katika nchi hiyo hawezi kupoteza uraia wake.
Akizungumza na Sauti ya Amerika kwa njia ya simu siku ya Jumapili kabla ya kuabiri ndege mjini London akiwa njiani kwelekea Kenya, Miguna alisema hakuna mtu yeyote aliye na nguvu kuliko amri ya mahakama, na kupuzilia mbali kauli zilizokuwa zikitolewa kwamba huenda seriakli isimruhusu kuingia nchini Kenya, licha ya mahakama kuamuru asizuiliwe kuingia na kwamba arejeshewe hati yake ya kusafiria.
“Ninasafiri na pasipoti yangu ya Canada kwa sababu mahakama iliamuru iwapo watakataa kurudisha cheti cha kusafiria, nina uhuru wa kutumia pasipoti ya Canada kusafiria. Nitaenda huko na sitaomba viza kwa sababu mahakama ilisema hivyo,” alisema Miguna.
Serikali ya Kenya haijatoa kauli yoyote hadharani kuhusu kurudi kwa mwanasiasa huyo ambaye aliwania nafasi ya gavana wa Nairobi kwenye uchaguzi wa mwaka jana.
Safari yake inajiri chini ya wiki tatu baada ya rais wa nchi hiyo Uhuru Kenyatta Kukutana na kiongozi wa upinzani Raila Odinga na kukubaliana kushirikiana pamoja kutafuta uwianio wa kitaifa.
Miguna alikuwa amekamatwa na kuzuiliwa na polisi kwa takriban siku tano kwa tuhuma kwamba alitoa kiapo – kinyume na sheria – kwa kiongozi wa upinzani, Raila Odinga, mbali na kuwa mwanachama wa vuguvugu la NRM lililopigwa marufuku.
Lakini licha ya mahakama moja mjini Nairobi kumtaka afikishwe mbele ya jaji, polisi walimuwasilisha mbele ya hakimu katika mji ulio mbali na mji mkuu wa Kenya, na baadaye wakampeleka moja kwa moja hadi kwenye uwanja wa ndege, na kuwondosha nchini.
Tangu wakati huo, Miguna amekuwa akishiriki mahojiano na vyombo mbalimbali vya habari na kufanya mikutano na Wakenya wanaoishi nje ya nchi, ikiwa ni pamoja na kutembelea miji kadhaa ya Canada, Marekani na Uingereza.
Tangu Miguna aondoke nchini, mgawanyiko mkubwa ndani ya muungano wa National Alliance Super Alliance (NASA) umejidhihirisha huku baadhi ya vinara wakuu wakisema kuwa Odinga aliwasaliti na kuashiria kwamba huenda muungano huo unaelekea kusambaratika.
Moses Wetangula, ambaye ni mmoja wa vinara wanne wa muungano huo, alisema yafuatayo siku ya Jumamosi: “Kile walizungumza, hakutuambia. Kile alipewa hakutuambia.”
Wetangula tayari amevuliwa madaraka ya kiongozi wa walio wachache kwenye seneti ya Kenya, na wadhifa huo ukachukuliwa na wakili wa chama cha Raila Odinga, ODM, ambaye pia ni seneta wa kaunti ya Siaya, James Orengo.
“Wanachama wa NRM wako tayari kuhakikisha kwamba hakuna shughuli zitakazoendelea katika mji wa Nairobi hadi pale wanyanyasaji wa raia walionykua madaraka kwa nguvu waachie mamlaka na kukubali kufanyika kwa uchaguzi huru na wa haki nchini Kenya,” Miguna aliuambia mkutano aliohutubia mjini London siku ya Ijumaa.
Hata hivyo, baadhi ya wachambuzi wa masuala ya sisasa wanasema hata ikiwa Miguna Miguna hatazuiliwa kuingia nchini Kenya, huenda ikawa vigumu kwake kutimiza malengo ya vuguvugu la NRM, hususan kufuatia mabadiliko makubwa ya Kisiasa yaliyotokea tangu aende uhamishoni.
Tayari Miguna amemkosoa vikali Raila Odinga kwa kukubali kushirikiana na rais Kenyatta huku akidai kwamba itakuwa vigumu mno kwa masuala waliokuwa wakipigania kama upinzani kutekelezwa.