Waziri wa ulinzi wa Ufaransa, amesema mitandao ya idara za ulinzi za nchi zilishambuliwa mara 24,000 mwaka jana peke yake lakini udukuzi huo ulizimwa.
Jean Yves-Le Drian, alisema udukuzi kama huo unaongezeka mara dufu kila mwaka.
Alionya kuwa miundo mbinu ya taifa iko kwenye hatari, na kwamba kunaweza kufanywa jaribio la kuchafua uchaguzi wa mwaka huu.
Bwana Le Drian amekuwa akisimamia mabadiliko makubwa katika mifumo ya mitandao ya Ufaransa, ambapo mkuu wa jeshi ataongoza operesheni mpya za komputa, Cybercom.
Waziri huyo wa ulinzi alisema hayo alipozungumza na gazeti moja la Ufaransa, Le Journal du Dimanche, baada ya idara za usalama za Marekani, kusema kuwa Urusi ilijaribu kuingilia kati uchaguzi wa rais wa Marekani jambo ambalo Urusi inakanusha.