MKUTANO wa tatu wa dharura kujadili mzozo na mkwamo wa kisiasa nchini Burundi uliosababisha maelfu ya raia kuitoroka nchi hiyo umeanza leo jijini Dar es salaam.
Viongozi hao wakiwemo mwenyekiti na mwenyeji wa jumuiya, rais Jakaya Kikwete wa Tanzania, na Yoweri Museveni wa Uganda, ambao tayari wamewasili kwenye kikao hicho, wanajadili na kuwasilisha mapendekezo ya ripoti mbili kuhusu mgogoro wa Burundi.
Ripoti hizo ni pamoja na ya kikosi cha pamoja cha kimataifa cha Usuluhishi wa mgogoro wa Burundi, kinachojumuisha, Umoja wa Afrika, na Umoja wa mataifa, jumuiya hiyo ya Afrika mashariki, pamoja na kikosi cha kimataifa kuhusu eneo la maziwa makuu. Pamoja na ripoti ya baraza la mawaziri wa Afrika Mashariki.