Mngereza aeleza alivyochangamkia mchongo wa TACIP, ‘inaongeza thamani’

Mngereza aeleza alivyochangamkia mchongo wa TACIP, ‘inaongeza thamani’

Like
718
0
Tuesday, 18 December 2018
Local News

Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), Godfrey Mngereza amejivunia kujiandikisha kwenye Mradi wa Utambuzi wa Wasanii wa Sanaa za Ufundi Tanzania (TACIP), ambao amedai umemuongezea thamani kama msanii.

Akizungumza na Dar24 katika mahojiano maalum, Mngereza ameeleza kuwa akiwa kama msanii wa sanaa ya ufundi pamoja na muziki, mbali na kuwa Katibu Mtendaji, ameamua kuchangamkia fursa ya TACIP kwani inaongeza thamani ya msanii na kumfanya aheshimike kwa kumtambulisha.

“Mimi ninazungumza kama Katibu Mtendaji, lakini nikiuvua ukatibu mtendaji mimi ni msanii. Nimesomea sanaa ya uchoraji na sanaa ya muziki, nilishafanya shughuli za kuchonga… lakini hapa tunazungumzia sanaa ya ufundi,” alisema Mnengereza.

“Ukitambulika hadhi yako inapanda, kwa sababu hadhi ya mtu, utambulisho wa mtu ni kitu cha msingi sana. Kwa sababu usipokuwa na utambulisho mtu anaweza kukudharaudharau tu. Lakini kumbe uchoraji, uchongaji, ususi, uchoraji ni kazi ya hali ya juu sana. Mimi nimeona fursa…. ndio nimejiandikisha (TACIP),” aliongeza.

Kadhalika, Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, Pili Ngarambe ambaye alizindua utekelezaji wa mradi wa TACIP katika halmashauri hiyo alisema kuwa mradi huo ni fursa ya kipekee kwa wasanii.

Alisema kuwa mradi huo unaunga mkono juhudi za Rais John Magufuli ambaye hivi karibuni amewapa wafanyabiashara wadogo vitambulisho ili waweze kutambulika na kuwa rasmi, kwani kuwa tambua wasanii ni wakuwaongezea heshima na kuwapa fursa zaidi.

Aliipongeza kampuni ya DataVision International kwa kuanzisha na kuratibu mradi huo unaolenga kuwapa fursa nyingi ikiwa ni pamoja na sifa za kukopesheka kwa kutumia kitambulisho cha TACIP.

TACIP ni mradi wa utambuzi wa Wasanii wa Sanaa za Ufundi nchini ambao umeanzishwa na kampuni ya kizawa ya Data Vision International iliyoko jijini Dar es Salaam, inayojishughulisha na Teknlolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), Tafiti na Mafunzo, ambapo wanatekeleza mradi huo kwa kushirikiana na Shirikisho la Sanaa za Ufundi Tanzania (TAFCA). Mlezi wa mradi huo ni Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *