Mpinzani atangazwa mshindi uchaguzi wa Urais DRC

Mpinzani atangazwa mshindi uchaguzi wa Urais DRC

Like
571
0
Thursday, 10 January 2019
Global News

Mgombea wa chama cha upinzani, Felix Tshisekedi ametangazwa kuwa mshindi wa uchaguzi wa Urais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), saa chache zilizopita.

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (CENI) kupitia kwa Mwenyekiti wake, Corneille Nangaa imemtangaza Tshisekedi kuwa amepata 38.5% ya kura zote akiwashinda wapinzani wake Martin Fayulu na aliyekuwa mgombea wa chama tawala Emmanuel Shadary.

Emmanuel Shadary aliyekuwa anaungwa mkono na Rais Joseph Kabila ameambulia nafasi ya tatu, huku mpinzani Fayulu akishika nafasi ya pili.

Kwa mujibu wa CENI, Tshisekedi  amepata kura milioni 7,  Fayulu amepata kura Milioni 6.4 na Shadary amepata kura Milioni 4.4.

Hata hivyo, Fayulu ameiambia Radio France kuwa hakubaliani na matokeo yaliyotangazwa kwa madai kuwa hayaendani na kura hasili zilizopigwa.

Tshisekedi anakuwa mpinzani wa kwanza nchini humo kushinda katika uchaguzi wa Urais, na huu ukiwa ni uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasia unaoshuhudia ubadilishanaji wa madaraka tangu nchi hiyo ipate uhuru kutoka kwa Ubelgiji mwaka 1960.

Hii ni hatua ya kihistoria ya chama cha UDPS amabacho kilikuwa kikiongozwa na baba yake Tshisekedi kwa miongo kadhaa, kilichokuwa kikijaribu kuongoza Serikali ya DRC bila mafanikio.

Matokeo hayo yaliyotangazwa saa chache zilizopita, awali yalikuwa yanatarajiwa kutangazwa Jumapili lakini CENI ilieleza kuwa haikuwa imekamilisha zoezi la kukusanya kura na kuzijumlisha kutoka kwenye vituo kadhaa.

Uwepo wa ulinzi mkali nje ya ofisi za CENI jana uliibua taharuki kwa wengi waliodai huenda matokeo yanayotakiwa kutangazwa ni kinyume na yanayotarajiwa na wananchi walio wengi.

Rais Kabila anatarajiwa kuachia rasmi madaraka mwezi huu, baada ya kuapishwa kwa Tshisekedi kuwa Rais Mpya wa tano wa nchi hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *