Msanii Judith Wambura ‘Lady Jaydee’ ameula katika michuano ya Kombe la Dunia 2014 baada ya kupata nafasi ya kuandaa wimbo kwa a jili ya michuano hiyo mikubwa zaidi ya soka duniani.
Jaydee anayefahamika pia kama Komandoo au Anaconda, amepata fursa ya kuandaa wimbo maalum wa michuano hiyo ‘FIFA World Cup Anthem’ akishirikiana na wakali wawili David Correy wa Brazil na rapa Octopizzo wa Kenya.
Katika wimbo huo, Lady Jaydee na Correy wameimba kwa lugha ya Kiingereza huku Octopizzo ‘akichana’ kwa Kiswahili.
Wimbo huo ulipigwa kwa mara ya kwanza jana jijini Dar es Salaam wakati kampuni ya Coca-Cola ilipozindua promosheni yake mpya ya miezi miwili ya Kombe la FIFA la Dunia 2014 ambayo itawawezesha wateja wake kujishindia zawadi mbalimbali zikiwamo tiketi za kwenda kushuhudia mechi za robo fainali za Kombe la Dunia nchini Brazil.
Meneja Mkazi wa Coca-Cola Tanzania, Yebeltal Getachew alisema hayo wakati wa hafla ya uzinduzi ya kampeni hiyo iliyofanyika jijini Dar es Salaam huku akizitaja zawadi nyingine kuwa luninga, mipira na fulana. Wakati huo huo, Jmosi tarehe 12 April Lady Jaydee anataraji kuachia wimbo wake na video mpya ‘Nasimama’.
CHANZO: Nipashe