SHIRIKA la madaktari wasio na mipaka-MSF, limerudia kutoa ombi la kufanyika uchunguzi huru, mwezi mmoja baada ya hospitali yake nchini Afghanistan kushambuliwa na ndege za kivita za Marekani.
Shirika hilo lenye makao yake mjini Paris, jana limefanya mkutano wake mjini New York na kutumia dakika moja kukaa kimya kuwakumbuka watu 30 waliouawa katika shambulizi hilo la anga, lililofanyika kwenye hospitali ya watu walioathirika na vita mjini Kunduz.
Mkurugenzi Mtendaji wa MSF Marekani, Jason Cone, amesema wamekuwa wakifanya kazi katika mazingira ya hatari hasa kwenye maeneo ya vita, ambapo Rais Barack Obama wa Marekani aliomba radhi na kusema shambulizi hilo limefanyika kwa bahati mbaya.