Mwana anga wa Marekani Gene Cernan, aliyekuwa binadamu wa mwisho kutembea kwenye Mwezi, amefariki dunia akiwa na miaka 82.
Shirika la anga za juu la Marekani Nasa limesema limehuzunishwa sana kumpoteza mwana anga huyo mstaafu.
Cernan alikuwa mmoja wa watu watatu pekee waliowahi kwenda Mwezini mara tatu na ndiye binadamu aliyeukanyaga Mwezi mara ya mwisho kabisa, mwaka 1972.
Maneno yake ya mwisho aliyoyasema kabla ya kuondoka kwenye Mwezi yalikuwa: “Tunaondoka jinsi tulivyokuja na, Mungu akitujalia, tutarejea na amani na matumaini kwa binadamu wote.”
Alikuwa kamanda wa chombo cha anga za juu cha Apollo 17 wakati huo.
Ni watu 12 pekee waliowahi kutembea kwenye Mwezi, na kati yao ni sita pekee ambao bado wako hai.