Mwana wa mlanguzi mkuu wa mihadarati nchini Mexico Joaquin El Chapo Guzman ni miongoni mwa washukiwa wa uhalifu waliotekwa nyara katika mji uliopo pwani ya Pacific siku ya Jumatatu kulingana na maafisa.
Wanasema kuwa Jesus Alfredo Guzman mwenye umri wa miaka 29 ni miongoni mwa wanachama sita wa genge la Sinaloa waliotekwa nyara na genge pinzani ,kwa jina Jalisco New Generation.
Kisa hicho kilitokea katika mkahawa uliopo mji wa kitalii wa Puerto Vallarta.
Chapo Guzman ambaye anahudumia kifungo ,aliliongoza genge hilo la Sinaloa kwa miaka kadhaa.
Jesus Alfredo anashukiwa kuwa mwanachama mkuu wa genge hilo.
Anatafutwa kwa mashtaka ya mihadarati na Marekani .
Marekani pia inamtaka Joaquin El Chapo Guzman kupelekwa nchini humo kwa mashtaka ya kusafirisha mihadarati mingi.
Alikamatwa kwa mara nyengine mnamo mwezi Januari ,miezi sita baada ya kutorokea kupitia bomba la kilomita 1.6 kutoka jela aliokuwa amefungwa.