Mwanamuziki XXXTentacion auawa kwa kupigwa risasi Florida, Marekani

Mwanamuziki XXXTentacion auawa kwa kupigwa risasi Florida, Marekani

Like
935
0
Tuesday, 19 June 2018
Global News

Mwanamuziki wa nyimbo za rap Marekani XXXTentacion, ambaye alipata umaarufu kwa haraka kupitia albamu zake mbili ameuawa kwa kupigwa risasi akiwa na miaka 20.

Alikuwa anaondoka kwenye duka la kuuza pikipiki kusini mwa Florida Jumatatu pale mtu mwenye bunduki alipomfyatulia risasi.

Polisi katika tarafa ya Broward wanasema XXXTentacion, ambaye jina lake Jahseh Onfroy, alikimbizwa hospitalini lakini akathibitishwa kufariki.

Alikuwa mara nyingi akielezwa kama mmoja wa wanamuziki wa rap wenye kuzua utata zaidi.

Alikuwa pia amekabiliwa na mashtaka ya kumshambulia mpenzi wake.

Rapa huyo, ambaye alipata umaarufu kwa kupakia nyimbo zake katika mtandao wa SoundCloud, alikuwa anatazamwa na wengi kama kielelezo cha mtu kufanikiwa kupitia kipaji chake.

Wapenzi wa muziki wake na wanamuziki nyota wa hip-hop wamekuwa wakituma salamu za rambirambi kuomboleza kifo chake.

Liwali wa tarafa hiyo amesema Onfroy alikuwa anaondoka kwenye duka hilo muda mfupi kabla ya saa kumi alasiri pale washukiwa wawili waliokuwa na silaha walipofika kwake.

Mmoja wao anadaiwa kumpiga risasi kabla ya wote wawili kukimbia eneo la tukio Deerfield Beach, takriban maili 43 (69km) kaskazini mwa Miami wakitumia gari aina ya SUV la rangi nyeusi.

Wachunguzi wanasema huenda kilikuwa kisa cha wizi wa mabavu.

Video iliyopakiwa kwenye mitandao ya kijamii ilimuonesha mwanamuziki huyo akiwa amelala ndani ya gari lake baada ya kupigwa risasi.

Mmoja wa walioshuhudia ameambia tovuti ya TMZ kwamba milio kadha ya risasi ilisikika nje ya duka hilo.

Rapa huyo, ambaye nyimbo zake ni pamoja na SAD! na Moonlight, zilipata umaarufu sana baada yake kutoa albamu yake ya kwanza kwa jina 17 Agosti mwaka jana.

Alitoa albamu nyingine kwa jina ? ambao ilianza ikiwa kwenye chati ya nyimbo 200 maarufu mwezi Machi na nyimbo za albamu hiyo zilikuwa zimesikizwa mara milioni mia kadha mtandaoni.

Alizungumzia mambo kama vile mfadhaiko na msongo wa mawazo na alisifiwa na baadhi ya wanamuziki nyota wa rap.

Lakini uimbaji wake ulikumbwa na utata, huku akituhumiwa kwa makosa ya kuwashambulia na kuwapiga watu.

Alikuwa anakabiliwa na mashtaka 15 ya kuwashambulia watu kufikia wakati wa kifo chake, shtaka moja likiwa la kumpiga mwanamke mja mzito.

XXXTentacion alikulia katika maisha ya dhiki na alifukuzwa shuleni kwa sababu ya kupigana, lakini alielekeza nguvu zake na ghadhabu kwenye muziki.

Kufikia Oktoba, alikuwa ametia saini mkataba wa muziki uliodaiwa kuwa wa dhamani ya $6 milioni (£4.5m).

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *