LEO zimetimia siku 500 tangu wanafunzi zaidi ya 200 wa kike walipotekwa nyara na kundi la kigaidi la Boko Haram kutoka mji cha Chibok kaskazini-mashariki mwa Nigeria, huku matumaini ya kupatikana kwa wanafunzi hao yakizidi kufifia.
Kumbukumbu hiyo inafanyika wakati hali ya usalama ikizidi kuwa mbaya katika eneo hilo, ambako Boko Haram wamezidisha mashambulizi tangu kuingia madarakani kwa rais Muhammadu Buhari, ambapo wameuwa zaidi ya watu 1,000 katika miezi mitatu.
Wapiganaji hao walivamia shule ya serikali mjini Chibok katika jimbo la Borno jioni ya Alhamis 14 mwaka jana, na kuwateka wanafunzi 276 waliokuwa wanajiandaa na mitihani yao ya mwisho wa mwaka.