Kiongozi wa kanisa Katoliki duniani Papa Francis amechukua hatua isiyotarajiwa na kuingilia kati kujaribu kutatua mzozo wa kisiasa nchini Venezuela.
Taifa hilo pia linakabiliwa na matatizo ya kiuchumi.
Wakati wa mkutano wa faraghani na Rais Nicolas Maduro uliofanyika Vatican, Papa Francis ameomba kuongoza mashauriano kati ya rais huyo na viongozi wa upinzani.
Mjumbe wa Papa nchini Venezuela Emil Paul Tscherrig amesema pande zote mbili zimeahidi kufanya mashauriano rasmi Jumapili ijayo katika kisiwa cha Margarita, Venezuela.
Lakini kupitia taarifa iliyopeperushwa mtandaoni, kiongozi wa upinzani Henrique Capriles amesema hakuna mazungumzo yoyote yaliyoanza na kwamba tangaza la kuanza upya kwa mashauriano ni njama ya serikali.
Wasiwasi umekuwa ukitanda Venezuela kutokana na kuahirishwa kwa kampeni za kura ya maoni ya kuamua kuhusu kuondolewa madarakani kwa Bw Maduro.