Papa Francis awataka vijana duniani kuinua sauti zao

Papa Francis awataka vijana duniani kuinua sauti zao

Like
312
0
Sunday, 25 March 2018
Global News

Papa Francis

Kiongozi mkuu wa kanisa la Katoliki, Papa Francis, Jumapili aliwashauri vijana duniani kuendelea kutetea masuala wanayoyaamini, na kutokubali sauti zao kuzimwa.
Akizungumza wakati wa ibada ya Jumapili ya matawi, Palm Sunday, iliyofanyika kwenye ukumbi wa St Peters Square mjini Vatican, Papa Francis aliwataka vijana kuendelea kupaza sauti zao hadi zitakaposikika.

Kauli yake imejiri siku moja baada ya maandamano makubwa kufanyika ulimwenguni kote siku ya Jumamosi kuishinikiza Marekani kuunda sheria zinazodhibiti umiliki wa bunduki hatari.

Hata hivyo, Papa Francis hakutaja maandamano hayo moja kwa moja, lakini alisema ni wajibu wa vijana kutonyamazia masuala wanayoyaamini.

Ibada ya Palm Sunday huashiria kuingia kwa Yesu Kristo kwa ujasiri mjini Jerusalem Zaidi ya miaka 2000 iliyopita na mwanzo wa wiki takatifu ya Pasaka kwa Wakristo.

Jumapili ya matawi wiki hii imeadhimishwa pamoja na siku ya Vijana Duniani.

Jumaosi, Mamilioni ya watu waliandamana katika miji mbalimbali ulimwenguni kote siku ya Jumamosi kushinikiza mageuzi katika sheria zinzohusu umiliki wa bunduki.

Kilele cha maandamano hayo yaliyopewa jina la March for our lives, ulikuwa ni mkutano uliohudhuriwa na takriban watu nusu milioni katika mji mkuu wa Marekani, Washington DC.

Maandamano hayo yalipangwa na shule ya upili ya Marjorie Stoneman Douglas mjini Parkland, jimbo la Florida, ambako watu wapatao 17, wakiwemo wanafunzi 14 walipoteza maisha yao kufuatia shambulizi la bunduki kwenye shule hiyo mapema mwaka huu.

Zaidi ya maandamano 800 yalikuwa yamepangwa kufanyika katika miji kadhaa ya Marekani na sehemu nyingine duniani kote, sambamba na yale ya mjini Washington DC.

Mashambulizi ya kutumia bunduki zenye nguvu, hususan kwenye shule Marekani yamezua mjadala mkali, huku wanasiasa wakitofautiana kuhusu hatua za kudhibiti matukio hayo.

Wanaharakati na wasanii maarufu walihudhuria maandamano hayo, wakiwemo wanamuziki Jennifer Hudson, Ariana Grande, Demi Lovato na Miley Cyrus.

Mjukuu wa mtetezi maarufu wa haki za binadamu Martin Luther King Jr, alishangiliwa kwa shanwe na vigelegele aliposimama kuhutubia mkutano wa Washington. Yolanda Renee King III alisema kizazi cha sasa ndicho kitaleta mabadiliko yanayohitajika.

“Na itoshe! Na itoshe!” alisema msichana huyo.

Kundi kubwa la waandamanaji baadaye lilionekana nje ya ikulu likibeba mabango licha ya kuwa rais Donald Trump hakuwemo wakati huo. Baadaye waliyaweka mabango yao chini na kuyaacha nje ya uzio wa ikulu kama ishara kwamba walitaka rais Trump asome ujumbe wao.

Comments are closed.