RAIA WA NIGERIA ALIYEKUTWA NA BANGI KUNYONGWA SINGAPORE

RAIA WA NIGERIA ALIYEKUTWA NA BANGI KUNYONGWA SINGAPORE

Like
246
0
Thursday, 17 November 2016
Slider

Singapore imekataa ombi la msamaha kutoka kwa raia mmoja wa Nigeria ambaye amepangiwa kunyongwa Ijumaa kwa kupatikana na bangi, shirika la haki za kibinadamu la Amnesty International limesema.

Familia ya Chijoke Stephen Obioha ilifahamishwa kuhusu hatua hiyo Jumatano.

Obioha alipatikana na kilo 2.6 za bangi Aprili 2007, kiasi kilichokuwa kimezidi kipimo cha gramu 500 ambacho mara moja humfanya mtu kuhukumiwa kwa ulanguzi wa dawa za kulevya chini ya sheria za Singapore.

Afisa wa Amnesty International Rafendi Djamin amesema shirika hilo limeshangazwa na hatua hiyo ya Singapore kumnyima mshtakiwa huyo msamaha.

Hata hivyo, alisema shirika hilo bado lina matumaini kwamba Singapore haitatekeleza adhabu hiyo “katili na isiyoweza kubatilishwa dhidi ya mtu huyo aliyehukumiwa kifo kwa kosa ambalo halifai adhabu ya kifo.”

“Hukumu ya kifo si suluhu. Haitaangamiza dawa zote za kulevya Singapore. Kwa kuwanyonga watu kwa makosa ya kuwa na dawa za kulevya, ambayo hayafikii kiwango cha makosa makubwa ya uhalifu, Singapore inakiuka sheria za kimataifa.

“Mataifa mengi ulimwenguni yameacha adhabu hii ya kikatili, kinyama na ya kudunisha.”

Comments are closed.