Rais Magufuli Atoa Wito kwa Majeshi Yote Nchini

Rais Magufuli Atoa Wito kwa Majeshi Yote Nchini

Like
813
0
Thursday, 17 May 2018
Local News

Rais Magufuli Atoa Wito kwa Majeshi Yote Nchini

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 17 Mei, 2018 amezindua kituo cha uwekezaji cha Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kilichopo katika kikosi cha Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Mgulani (831KJ) Jijini Dar es Salaam.

Kituo hicho kina viwanda vya kushona nguo, kutengeneza maji, kukereza vyuma na pia kina chuo cha ufundi stadi (VETA), shule ya sekondari Jitegemee na kumbi mbili za mikutano (Muhuga Hall na Isamuhyo Hall). Uwekezaji wote umegharimu Shilingi Bilioni 5 na Milioni 793.

Pamoja na kuzindua kituo hicho Mhe. Rais Magufuli ametembelea kiwanda cha ushonaji wa nguo kilichogharimu Shilingi Milioni 810 na ambacho kina uwezo wa kushona jozi 500 za sare za askari kwa siku na kuzalisha ajira za watu 350, na pia ametembelea kiwanda cha kutengeneza maji ambacho kimegharimu Shilingi Bilioni 1 na Milioni 600 na kina uwezo wa kuzalisha chupa 3,600 za maji kwa saa.

Akizungumza katika mkutano uliohudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Mawaziri, Makatibu Wakuu, Maafisa Wakuu na Askari wa JWTZ, Wakuu wa Majeshi wastaafu na Majenerali wastaafu, Mhe. Rais Magufuli ameipongeza JWTZ kupitia Shirika lake la SUMAJKT kwa kuitikia vizuri wito wake wa kujenga viwanda na ameahidi kuwa Serikali itaendelea kutoa ushirikiano mkubwa kwa JWTZ katika jukumu hili la kujenga uchumi wa nchi kupitia viwanda na shughuli nyingine za uzalishaji mali.

“Naomba nimpongeze Meja Jenerali Mstaafu Michael Isamuyo kwa jitihada alizozifanya kujenga miradi hii akiwa Mkuu wa JKT, nampongeza Mkuu wa JKT wa sasa na SUMAJKT kwa kazi nzuri mnayoifanya, kwa kweli leo nimefurahi sana kuona jeshi letu linajenga viwanda, huu ni mwelekeo mzuri, askari wetu sasa watashonewa nguo kutoka hapa hapa nchini kwetu” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Mhe. Rais Magufuli ametoa wito kwa majeshi yote nchini kununua sare kutoka viwanda vya majeshi na kwa upande wa maji ametoa wito kwa Watanzania kunywa maji ya Uhuru Peak yanayotengenezwa na SUMAJKT zikiwemo ofisi za umma, na amebainisha kuwa uwekezaji huo utasaidia JWTZ kupata mapato kwa ajili ya kujiendesha na kupunguza ukubwa wa fedha za bajeti kutoka Serikalini.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli ametoa muda wa mwezi mmoja kwa taasisi za Serikali, taasisi binafsi na watu binafsi waliokopeshwa matrekta kupitia SUMAJKT na hawajarejesha Shilingi Bilioni 38 mpaka sasa, na taasisi za Serikali zinazodaiwa na SUMAJKT Shilingi Bilioni 3.4 kutokana na kutolipia huduma za ulinzi, kulipa madeni hayo vinginevyo vyombo vya dola viwakamate wadaiwa wote popote walipo.

“Jen. Mabeyo nimekusikia juu ya madeni mnayodai, nataka ndani ya mwezi mmoja madeni haya yawe yamelipwa, najua mkipata fedha hizi mtaweza kujenga viwanda vingine ili tuendelee kuzalisha ajira kwa Watanzania na kujenga uchumi wetu” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.

Mapema akitoa taarifa kwa Mhe. Rais Magufuli, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jen. Venance Salvatory Mabeyo ameishukuru Serikali kwa kuunga mkono jitihada za jeshi hilo kujenga viwanda na amemhakikishia kuwa JWTZ imedhamiria kutekeleza maagizo ya Mhe. Rais ambapo kupitia mashirika yake ya Mzinga Corporation, Nyumbu Project na SUMAJKT imekamilisha viwanda vya kuchakata nafaka vya Mlale JKT na Mafunga JKT, Kiwanda cha kuchakata kahawa cha Itende JKT na inaendelea kujenga kiwanda cha mafuta ya kula cha Kigoma.

Ameongeza kuwa JWTZ inategemea kujenga kiwanda cha chumvi katika eneo la Msindo Kilwa Masoko, na kwamba ipo tayari kushirikiana na taasisi za ndani na nje ya nchi kujenga viwanda zikiwemo mifuko ya hifadhi ya jamii ya NSSF na PPF katika mradi mkubwa wa uzalishaji wa sukari wa Mkulazi, na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ambako wataanzisha kiwanda cha maji tiba (Intravenous Fluid).

Kwa upande wake Waziri wa Ulinzi na JKT Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema mazungumzo na nchi ya Misri yamekwenda vizuri ambapo kwa ushirikiano na JWTZ wataanzisha kiwanda cha dawa, kujenga machinjio na kiwanda cha kuchakata nyama, wakati Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe. Charles Mwijage amesema kujengwa kwa kiwanda cha maji ya Uhuru Peak kunafanya Tanzania iwe na jumla ya viwanda vya maji 67 vilivyojengwa kuanzia mwaka 2015 na ambavyo vimezalishaji ajira 6,000, vimelipa kodi Shilingi Bilioni 59.7 na vimefanikiwa kutosheleza mahitaji nchini.

 

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Dar es Salaam

17 Mei, 2018

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *