Rais wa Ukraine Petro Poroshenko ameiomba Nato kutuma meli kwenda bahari ya Azov kufuatia makabiliano yaliyotokea kati ya Ukraine na Urusi baharini eneo la Crimea.
Poroshenko aliliambia gazeti la Ujerumani Bild kuwa anaamini kuwa meli hizo zitapelekwa “kuisaidia Ukraine na kuweka ulinzi”.
Siku ya Jumapili Urusi ilivamia meli tatu za Ukraine na kuwashika mabaharia wake kutoka Kerch strait.
Nato imesema inaunga mkono Ukraine ambayo si mwanachama wake.
Siku wa Jumatano Rais wa Urusi Vladimir Putin alimlaumu Bw Poroshenko kwa kuanzisha uhasama wa baharini ili kujiongeze umaarufu kabla ya uchaguzi wa mwaka 2019.
Rais Poroshenko alitanga sheria ya kijeshi sehemu za mpaka wa Ukraine kwa siku 30 kama jibu kwa mzozo huo.
Wakati wa mahojiano na Bild, Bw Poroshenko alisema Vladimir Putin alikuwa na mpango wa kudhibiti bahari ya Azov.
“Ujerumani ni mmoja wa washirika wetu wa karibu sana na tunamatumaini kuwa nchi kwenye Jumuiya ya Nato sasa ziko tayari kupeleka meli katika bahari ya Azov ilia kuisaidia Ukraine kuweka ulinzi,” alisema.
“Hatuwezi kukubali sheria hii ya uchokozi ya Urusi. Kwanza ilikuwa ni Crimea, kisha mashariki mwa Ukraine, na sasa anataka bahari ya Azov. Ujerumani pia inastahili kujiuliza: Ni kipi tena Putin atafanya kama hatuwezi kumzuia?”
Siku ya Jumatatu, mkuu wa Nato Jens Stoltenberg alitoa wito kwa Urusi kuziachilia meli za Ukraine na kusema ni lazima Urusi ijue kuwa kuna madhara kwa vitendo vyake.
Alisema kuwa Nato itandelea kutoa msaada kwa Ukraine ambayo ni mshirika wa Nato, ingawa si mwanachama kamili.
Nato haikujibu mara moja taarifa za hivi punde kutoka kwa Bw Poroshenko.
Takriban wanajeshi watatu wa Ukraine walijeruhiwa wakati walinzi wa mpaka wa Urusi walifyatulia risasi boti mbili za kivita za Ukraine na boti nyingine ndogo karibu na Crimea.
Rasi hiyo ilimegwa kutoka Ukraine na Urusi mwaka 2014.
Boti hizo za jeshi la wanamaji zilikuwa safarini kutoka Odessa kwenda Mariupol, bandari ya Ukraine iliyo bahari ya Azov wakati zilikabiliwa na meli za walinzi wa mpakani wa Urusi.
Nchi zote zilikubalina kutumia kwa pamoja bahari mwaka 2003 lakini uamuzi wa Urusi kufungua daraja katia eneo la Kerch Strait mwaka huu imeibua msukosuko.
Ukraine inasema Urusi inafunga makusudi Mariupol na bandari nyingi ya Berdyansk kuzuia meli kupitia Kerch Strait.
Mabaharia 24 wa Ukraine walikamatwa na sasa wamepewa kufungo cha miezi miwili na mahakama huko Crimea.
“Bila ya shaka huu ni uchokozi,” rais wa Urusi alisema, akiongeza kwa “hii imepangwa na mamlaka za Ukraine. Na ninafikiria ni rais wa sasa kabla ya uchaguzi wa urais nchini Ukraine Machi mwaka 2019”.
Bw Poroshenko ana umaarufu mdogo. Kura za maoni za hivi majuzi zilionyesha kuwa ni asilimia 10 ya wapiga kura wanaopanga kumpigia kura mwaka ujao huku karibu asilimia 50 wakisema hawatampigia kura kwa vyovyote vile.
Alisisitiza kuwa jibu la jeshi la Urusi lilihitajika kwa kuwa Ukraine ilikuwa imevuka na kuinga maji ya Urusi.
Serikali za magharibi zimeunga mkono serikali ya Ukraine.
Siku ya Jumatano EU ililaani vikali vitendo vya Urusi lakini ikashindwa kukubaliana na vikwazo vipya dhidi ya Urusi.
Ilitoa wito kwa Urusi kuachilia meli hizo na mabaharia wake na kuheshimu uhuru wa Ukraine. Poland ilikuwa inataka vikwazo vipya dhidi ya Urusi huku Ujerumani na Ufaransa wakita misukosuko kutulizwa.