Rubani wa naibu rais William Ruto amefariki katika jali ya ndege baada ya helikopta aliyokuwemo kuanguka nchini Kenya.
Taarifa katika vyombo vya habari nchini zinaeleza kwamba ndege hiyo ilianguka Jumapili mwendo wa saa mbili usiku katika eneo la Turkana.
Inaarifiwa kwamba Kapteni Mario Magonga amefariki pamoja na abiria wengine wanne.
Polisi inasema helikopta hiyo imeanguka katika eneo la Labolo, kisiwa chenye milima ya volcano katikakati ya ziwa Turkana – Central Island National Park kaskazini magharibi mwa Kenya.
“Taarifa zilizopo zinaashiria kwamba ndege mbili zilitua mapema katika kambi ya Lobolo katika kisiwa hicho kilichopo kwenye mbuga ya kitaifa, hatahivyo moja ndio iliyofanikiwa kutua salama katika eneo hilo,” idara ya polisi imesema katika taarifa yake rasmi.
Inaarifiwa kwamba vikosi vya usalama vimetumwa katika eneo hilo katika kusaidia kwenye jitihada za kuondosha miili na masalio ya ndege hiyo.
Kufikia sasa, chanzo cha ajali bado hakijajulikana.
Alikuwa rubani wake naibu rais wa Kenya William Samoei Ruto.
Aliwahi kuwa rubani katika jeshi la Kenya.
Ni mzawa wa Nyamataro, Kitutu Chache kusini, kaunti ya Kisii – kusini magharibi mwa Kenya.
Babake ni mwanajeshi mstaafu; Brigedia (rtd) Magonga.
Alikuwa rubani mkuu wa helikopta za kampuni ya KIDL helicopters – inayotoa huduma za usafiri binafsi katika eneo zima la Afrika mashariki.
Alikuwa mkufunzi aliyehitimu wa helikopta.
Alipokea mafunzo kutoka kikosi cha ulinzi Kenya KDF.
Ana uzoefu wa kuendesha ndege kwa zaidi ya saa 5500 kwenye ndege za injini moja na injini zaidi ya moja.
Kwa waliofahamu, wanamueleza kuwa rubani aliye na taaluma na uzoefu mkubwa, na aliheshimika pakubwa.