SALVA KIIR, MACHAR KUKUTANA TANZANIA

SALVA KIIR, MACHAR KUKUTANA TANZANIA

Like
345
0
Monday, 20 October 2014
Global News
SUDAN

Wakaazi wa Sudan Kusini walioathiriwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe katika jimbo la Juba

Rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir na aliyekuwa makamu wake waliyehasimiana Riek Machar, leo wamealikwa kuhudhuria uzinduzi wa mazungumzo ya kutafuta muafaka ndani ya chama cha SPLM kinachoongoza taifa hilo lenye machafuko ya kisiasa.

Mazungumzo hayo yanatarajiwa kufanyika Arusha chini ya usimamizi wa CCM, chama tawala nchini Tanzania.

Endapo mahasimu hao wawili watafika na kukaa meza moja itakuwa ni hatua muhimu katika jitihada ambazo zimekuwa zikifanyika na jumuiya ya kimataifa kupata muafaka wa machafuko yanayoendelea katika taifa hilo changa kuliko yote barani Afrika.

Tangazo la kualikwa kwao lilitolewa na katibu wa Chama Cha Mapinduzi, Abdulrahman Kinana, baada ya mkutano wa siku tano uliofanyika Arusha kuandaa misingi itakayosimamia mazungumzo ya muafaka kufuatia maombi ya chama cha SPLM.

Mchakato huo unaosimamiwa na CCM unafanyika kuunga mkono jitahada zinazoendelea kumaliza mgogoro ambao mpaka sasa umesababisha vifo vya maelfu ya watu na wengine mamilioni kuyakimbia makazi yao.

Mazungumzo ya awali yaliwakutanisha wawakilishi kutoka SPLM KUU, SPLM UPINZANI na KUNDI LA WANACHAMA waliowahi kuwekwa kizuzini, lengo likiwa ni kuyaunganisha makundi hayo na kumaliza tofauti zao.

Viongozi hao inaaminika wataitikia wito wa Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania ambaye anafanya kazi hiyo kwa kofia ya mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi, CCM.

Na kama wakifika Arusha kukaa meza moja ya mazungumzo itakuwa ni hatua ambayo haijafanikiwa tangu watofautiane na machafuko kuzuka nchini Sudan Kusini mwezi Desemba mwaka jana.

Kwa miaka mingi Tanzania imekuwa mstari wa mbele kusaidia upatanishi barani Afrika, katika miaka ya karibuni imesaidia kumaliza mgogoro wa kisiasa nchini Kenya baada ya uchaguzi wa mwaka 2007 uliosababisha mauaji na maelfu ya watu kukimbia makazi yao.

Comments are closed.