SCHWEINSTEIGER ATHIBITISHA KUHAMIA UNITED

SCHWEINSTEIGER ATHIBITISHA KUHAMIA UNITED

Like
223
0
Monday, 13 July 2015
Slider

Bastian Schweinsteiger alithibitisha Jumapili kwamba ataondoka na Bayern Munich na kujiunga na Manchester United, ikitegemea matokeo ya uchunguzi wa afya yake, licha ya kwamba mabingwa hao wa Ujerumani wamepoteza mechi mbili zao za kwanza za kabla ya msimu wakicheza bila yeye.

Bayern walitangaza Jumamosi kwamba walikuwa wameafikiana kuhusu bei ya mchezaji huyo mwenye miaka 30, ambaye atafikisha kikomo kipindi chake cha miaka 17 katika klabu hiyo na kutia saini mkataba wa miaka mitatu na klabu hiyo ya Uingereza.

Kiungo huyo wa kati ambaye pia hutumiwa kama mkabaji alipakia kwenye Twitter picha yake akiwa ndegeni Jumapili yenye maelezo: “Ndoto moja ya mwisho katika uchezaji wangu itatimia. Nina furaha kuhusu sura mpya ijayo ya maisha yangu ya uchezaji nikiwa na Manchester United”.

“Mashabiki wapendwa, baada ya miaka 17 ya ufanisi FC Bayern, mataji 15 ya kitaifa, kushinda mataji matatu makuu msimu mmoja na mafanikio mengine, nimeamua kupiga hatua nyingine katika uchezaji wangu,” akaandika Schweinsteiger kwenye ukurasa wake wa Facebook.

“Uamuzi huu ulikuwa mgumu sana kuufanya kwa sababu nyinyi na FC Bayern mmekuwa, mko na daima mtakuwa sehemu muhimu ya maisha yangu.

“Hata hivyo, ningependa kupitia mapya katika klabu mpya na safari yangu yanielekeza Manchester United.

“Natumai mtaelewa uamuzi wangu. Hakuna anayeweza kufuta safari ambayo tumekuwa nanyi pamoja.”

Atakuwa Mjerumani wa kwanza kuchezea United.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari Ujerumani na Uingereza, United watawalipa Bayern takriban £14m (euro 19.47m, $21.72m) na hilo litapelekea Schweinsteiger kufanya kazi tena na mkufunzi wa zamani wa Bayern ambaye sasa ndiye meneja wa Manchester United Louis van Gaal.

Miamba hao wa Uingereza inadaiwa wanataka kukamilisha uhamisho huo haraka ili Schweinsteiger aweze kujiunga nao watakapoanza safari yao ya kuzuru Amerika kaskazini Jumatatu.

Comments are closed.