WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imedhamiria kumaliza tatizo la upatikanaji wa mafuta ya kula nchini kwa kufanya mageuzi makubwa katika zao la michikichi, alizeti na ufuta.
Ameyasema hayo leo (Jumatano, Juni 27, 2018) wakati akizungumza na Balozi wa Tanzania nchini Malaysia, Balozi Dkt. Ramadhan Dau ofisini kwake Mlimwa jijini Dodoma.
’’Tunataka kufanya mageuzi makubwa ya zao la michikichi, tunataka kuondoa miti ya zamani na kupanda miche mipya. Tutafanya kampeni ya kuhamasisha upandaji wa miche mipya ya michikichi ili tuondoe tatizo la upatikanaji wa mafuta nchini,’’.
Waziri Mkuu amesema licha ya kuwepo kwa michikichi mingi nchini ila uzalishaji wake unafanyika kwa njia kienyeji, hivyo Serikali imedhamiria kuboresha kilimo hicho kwa kutumia teknolojia ya kisasa ili liweze kuleta manufaa makubwa kwa Taifa na wakulima.
Amesema mbali na zao la michikichi, pia Serikali imedhamiria kuboresha mazao mengine ya mbegu za kukamua mafuta kama alizeti na ufuta, ambayo itayafuatilia kuanzia hatua za awali za uandaaji wa mashamba hadi masoko.
Kadhalika, Waziri Mkuu amesema Tanzania bado ipo chini kwenye uzalishaji wa mbegu za kukamulia mafuta na inahitaji wawekezaji katika mazao hayo, hivyo amemuagiza Balozi wa Tanzania nchini Malaysia atafute wawekezaji hao.
’’Inawezekana kujitosheleza kwa mafuta ya kula kwa sababu Tanzania tuna ardhi ya nzuri yenye rutuba na watu ambao kilimo ndiyo shughuli yao kubwa. Na hivi karibuni nitafanya ziara mkoani Kigoma kwenda kuhamasisha kilimo cha michikichi,’’.
Kwa upande wake, Balozi Dkt. Dau amesema Malaysia ndiyo nchi inayoongoza duniani kwa kilimo cha michikichi na inatengeneza zaidi bidhaa 400 kutokana na zao hilo, yakiwemo mafuta ya kuendeshea magari.
Balozi Dkt. Dau amemhakikishia Waziri Mkuu kwamba atatafuta wawekezaji kutoka nchi za Malaysia na Indonesia ili waje kuwekeza kwenye mashamba na viwanda vya mafuta na sukari.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
41193 – DODOMA.
JUMATANO, Juni 27, 2018.