Serikali yakerwa na vitendo vya mauaji na unyang’anyi mipakani

Serikali yakerwa na vitendo vya mauaji na unyang’anyi mipakani

Like
722
0
Wednesday, 20 February 2019
Local News

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameviagiza vyombo vya ulinzi na usalama kuongeza ulinzi na doria katika maeneo ya mipaka kutokana na ongezeko la vitendo vya mauaji, unyang’anyi wa kutumia silaha na vitisho kwa wananchi.

Ametoa agizo hilo alipokuwa akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa wilayani Kibondo wakati akihitimisha ziara yake mkoani Kigoma.

Pia, Waziri Mkuu ameagiza wakimbizi wote watakaobainika kutoroka kwenye makambi wanayohifadhiwa na kuingia uraiani wakamatwe na wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria za Tanzania, kwani wanachokifanya ni ukiukwaji wa sheria.

Aidha, maeneo yaliyo katika hali mbaya ni Kibondo, Buhigwe, Kasulu, Ngara, Biharamulo, Uvinza, Kakonko na Kigoma Vijijini, ambako wananchi hususani wafanyabiashara wameingiwa na hofu kutokana na vitendo hivyo.

”Kulinda usalama wa nchi ni jukumu letu sote na si la vyombo vya ulinzi na usalama pekee, kila mmoja anapaswa kushiriki. Kwa upande wa majirani zetu wanaotaka kuja nchini ni lazima wafuate taratibu kwa kuomba vibali.”amesema Majaliwa

Hata hivyo, Majaliwa ameongeza kuwa watu wote wanaoingia bila ya kufuata sheria na taratibu ndio hao wanashiriki katika vitendo vya uhalifu yakiwemo mauaji ya raia wasiokuwa na hatia, unyang’ani wa kutumia silaha za kivita pamoja na utekaji wa watoto.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *