SIMBA ACHENI VITA NA SINGANO, ELEKEZENI NGUVU KUIANDAA TIMU IBEBE MATAJI

SIMBA ACHENI VITA NA SINGANO, ELEKEZENI NGUVU KUIANDAA TIMU IBEBE MATAJI

Like
333
0
Monday, 13 July 2015
Slider

Na Omary Katanga.

Mzozo kati ya klabu ya Simba na mchezaji Ramadhani Singano “Messi” ndiyo habari iliyochukua nafasi kubwa kwenye vyombo vya habari kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa,huku kila upande ukidai kuwa na haki katika kile inachokiamini.

Hebu nikukumbushe kidogo mzozo huu ulipoanza,siku chache kabla ya dirisha la usajili kufunguliwa klabu ya Simba ilianza kupekuwa mikataba ya wachezaji wake kujua ni yupi mkataba wake umekwisha na yupi bado,ndipo jicho la upekuzi wao likanasa kwa mchezaji Ramadhani Saingano.

Hapo wakagundua kuwa muajiriwa wao huyo waliingia naye mkataba wa miaka mitatu na kutakiwa kuendelea kuitumikia klabu mpaka mwaka 2016,huku upande wa mchezaji mwenyewe ukibaini kuwa mkataba wake unaishia mwaka 2015.

Ndipo taratibu za kusuluhisha jambo hilo zikaanza kwenye mamlaka za shirikisho la soka TFF,lakini hatimaye kamati ya Katiba,Sheria,Maadili na Hadhi ya wachezaji ikamtangaza Singano kuwa mchezaji huru,uamuzi ambao Simba hawakuridhika nao na kupelekea mzozo huo kuchukua sura nyingine ya madai.

Hebu nirudi kwenu Simba,mimi sitaki kwenda mbali sana kwenye mambo ya kisheria kwa kuwa sina taaluma hiyo,lakini  kwakuwa uamuzi umetolewa na mamlaka yenye dhamana ya kusikiliza malalamiko kama hayo,hakuna budi kukubaliana nayo kwani si jambo la ajabu kwa klabu kushindwa kesi.

 

Itakumbukwa hata Yanga waliwahi kukumbwa na malalamiko kama hayo juu ya mchezaji wa kiganda Emanuel Okwi,ambaye aliamuliwa kuwa huru na baadaye akajiunga na Simba,lakini Uongozi wa Yanga ulikubali matokeo na kuamua kuweka silaha chini na wakaelekeza nguvu kwenye kuiandaa timu na hatimaye kuchukua ubingwa.

Jambo la msingi kwenu viongozi kwa sasa ni kuelekeza nguvu zenu kuiandaa timu na mikikimikiki ya ligi kuu na michuano ya FA,ili kuwakumbusha mashabiki wenu furaha ya kunyakua ubingwa wa bara, ambayo imepotea kwa miaka mitatu mfululizo.

Kwasasa kikosi chenu kinaongozwa na kocha mpya, Dylan Kerr (Muingereza) anayehitaji utulivu na ushirikiano toka kwa viongozi na mashabiki, ili ajue changamoto zilizopo kwenye klabu kiasi cha kushindwa kukamata nafasi mbili za juu kwa misimu mitatu iliyopita  kama ilivyo katika historia yake.

Simba ni klabu yenye historia kubwa katika soka la Tanzania tangu ilipoanzishwa mwaka 1936,lakini huwezi kuona ajabu watu wakiizungumzia kuwa ni klabu inayoendeshwa kiujanja ujanja licha ya kubalidisha viongozi wenye weledi tofauti.

Lakini nitoe angalizo kwa wachezaji wote,kuwa makini na kuwashirikisha wanasheria kabla ya kusaini mkataba na klabu yeyote,ili kujua haki zake za msingi na majukumu yake kwenye klabu.

Nimalizie kwa kuwatakia kila la heri timu ya taifa wanawake U-20 (Tanzanite) katika kibarua chao cha kwanza leo kwenye dimba la Chamazi dhidi ya Zambia ( She-Polopolo),kusaka tiketi ya michuano ya dunia.

Mwisho.

 

 

Comments are closed.