Baada ya kiungo Feisal Abdallah ‘Fei Toto’ kutambulishwa na Yanga jioni ya jana kwa kusainishwa mkataba wa miaka miwili, Uongozi wa Singida United umeibuka na kueleza kuwa hatima yake itaamuliwa na TFF pamoja na Bodi ya Ligi.
Mapema jana asubuhi ripoti kutoka Singida zilisema wamemalizana na Toto kwa kuingia naye mkataba wa miaka mitatu usio wa awali huku picha na video zikisambaa mitandaoni kuhusiana na usajili wake ndani ya Singida United.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Singida United, Festo Sanga, amefunguka na kueleza kuwa hatima ya usajili wake utaamuliwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) pamoja na Bodi ya Ligi kutokana na mamlaka kuwa kwao.
Sanga ameeleza kuwa wao walikuwa wameshamalizana kwa kila kitu na Toto ambaye alikuwa na wakala wake pamoja na Mwanasheria wakati wa kusaini mkataba huku akiwa amechukua sehemu kubwa ya fedha.
Kutokana na Yanga kumtambulisha jana jioni ikiwa ni saa kadhaa Singida wametoka kuweka wazi taarifa za kuwa mchezaji wao kwa miaka mitatu, Sanga amesema TFF itahusika na utatuzi wa suala hilo ambalo hata wao limewashangaza.
“Sisi tunachoamini kuwa mchezaji huyu amesaini Singida United na ameshachukua sehemu kubwa ya fedha, taratibu zote za usajili wake zilifuatwa hivyo TFF na Bodi ya Ligi tunawaachia hatima ya utatuzi wa suala hili” alisema Sanga.
Toto ametambulishwa jana na uongozi wa Yanga tayari ameshasaini mkataba wa miaka miwili baada ya kumalizana na JKU ya Zanzibar ambayo ipo kwenye mashindano ya KAGAME yanayoendelea hivi sasa Dar es Salaam.