Spika Ndugai aizungumzia hoja ya Bashe kuhusu mauaji na utekaji

Spika Ndugai aizungumzia hoja ya Bashe kuhusu mauaji na utekaji

Like
574
0
Thursday, 05 April 2018
Local News

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai amezungumza kuhusu taarifa za Mbunge wa Nzega Mjini kwa tiketi ya CCM, Hussein Bashe aliyetangaza kuwasilisha hoja binafsi Bungeni kuhusu matukio ya kiusalama nchini.

Katika mahojiano na kituo cha runinga cha Azam, Spika Ndugai amesema bado hawajapata taarifa rasmi kutoka kwa Bashe na kutoka kwa katibu wa wabunge wa CCM Bungeni kama kanuni zinavyoelekeza.

“Niliona barua yake kwa Katibu wa Bunge akimtaharifu kuwa anayo nia ya kuleta hoja binafsi lakini hiyo hoja yenyewe sijasikia kama ameiwasilisha sasa inakuwa vigumu sana kusema chochote juu ya jambo ambalo halijawasilishwa rasmi alichofanya ni kuwasilisha taarifa,” amesema.

Spika Ndugai ameongeza kuwa zipo kanuni za Bunge na zile za uendeshaji shughuli kwa wabunge wa CCM, vile kuna kanuni za kambi ya upinzani.

“Kwa yeye kama mbunge wa CCM, kanuni zinamtaka hoja yake aipeleke kule kwanza kwenye chama chake ikajadiliwe kule ikikubaliwa kule ndio tuweze kuipokea, kwa hiyo bado Bashe hajatuletea hiyo taarifa lakini bado hatujapata taarifa kutoka kwa katibu wa wabunge wa CCM Bungeni,” amesema Spika Ndugai.

Katika hatua nyingine Spika Ndugai amezungumza kuhusu hali yake ya kiafya ambapo hivi karibuni alirejea nchini kutoka kwenye matibabu.

“Namshurukuru Mungu sasa hali yangu ni bora zaidi kuliko ilivyokuwa hapo awali, nichukue nafasi hii kuwashukuru sana madaktari na wasaidizi wao wote na Watanzania kwa kuniombea na kunitakiwa kila na kheri,” amesema.

Comments are closed.