TEF watuma salamu za rambirambi, yataka elimu ya majanga iongezwe

TEF watuma salamu za rambirambi, yataka elimu ya majanga iongezwe

Like
490
0
Monday, 24 September 2018
Local News

 

Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) limetoa salamu za pole kwa Rais John Magufuli, familia, ndugu, jamaa na marafiki waliopoteza wapendwa wao katika ajali ya Kivuko cha MV Nyerere.

Salamu hizo zimetolewa Jana Septemba 23,2018 na Kaimu Mwenyekiti wa Jukwaa hilo, Deodatus Balile ambaye amesema wamepokea kwa mshituko taarifa za kupinduka kwa kivuko hicho.

Amesema ajali hiyo inarejesha kumbukumbu mbaya kwa Watanzania kwani inawakumbusha ajali za MV Bukoba iliyotolea Mei 21 mwaka 1996 katika Ziwa Victoria ambako watu zaidi ya 800 walipoteza maisha.

Amesema MV Spice Islander mwaka 2011 katika Bahari ya Hindi, ambako zaidi ya watu 200,walipoteza maisha, huku MV Skagit nayo ikizama kwenye bahari hiyo hiyo nakupoteza maisha ya watu karibu 150 mwaka 2012.

“TEF inatoa pole kwa Rais, familia za wafiwa, ndugu, jamaa na marafiki. Tunafikiri wakati umefika wa Tanzania kuzuia kuendelea kushuhudia majanga kama haya ambayo kwa hakika yanataka kugeuka kuwa utamaduni wa uendeshaji wa vyombo vya majini nchini,” amesema.

“Tunaisihi Serikali, wananchi na wadau mbalimbali kuongeza elimu ya udhibiti na tunaisihi Serikali, wananchi na wadau mbalimbali kuongeza elimu ya udhibiti wa majanga, huku tukijenga utamaduni wa kuheshimu sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa kwa usalama wa abiria,” amesema Balile.

Balile amesema wana imani utafanyika uchunguzi wa kina na waliohusika na uzembe huu uliogharimu maisha ya Watanzania watafikishwa katika vyombo vya sheria.

“Tunaomba katika kipindi hiki kigumu tuwe na utulivu, tuendeleze umoja na mshikamano wa Watanzania, huku tukivisihi vyombo vya dola vinavyofanya uchunguzi kuharakisha uchunguzi na kuwatendea haki waliohusika kwa mujibu wa sheria,” amesema.

Balile amesema, “Tunaomba Mungu awape nafuu manusura waliojeruhiwa na pumziko la milele Watanzania wenzetu waliopoteza maisha. Amina.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *