Maafisa nchini Urusi wamesema mwanafunzi mmoja amefanya mashambulizi katika chuo kimoja cha ufundi katika eneo la Crimea, wanafunzi 19 wameuwawa katika kadhia hiyo huku watu wengine na zaidi ya 40 walijeruhiwa.
Taarifa ya Sergei Aksyonov, kiongozi wa kikanda huko Crimea, ndio kauli ya hivi karibuni katika mfululizo wa maelezo yanayo badilika badilika kutok kwa maafisa wa Urusi kuhusu nini hasa kilichotokea katika Chuo cha ufundi kilicho katika mji wa pwani ya bahari nyeusi wa Kerch.
Maafisa hao kwanza waliripoti kwamba mlipuko wa gesi ulikua umetokea na kisha wakasema kuwa kulikuwa na mlipuko kwenye ukumbi wa maankuli katika chuo hicho uliohofiwa kuwa ni shambulio la kigaidi.
Lakini watu walioshuhudia tukio hilo wametoa taarifa kwamba baadhi ya watu waliuawa baada ya mshambuliaji kuwafyatulia risasi. Kiongozi huyo wa kikanda, Aksyonov amesema kwenye televisheni kuwa mwanafunzi, aliyewashambulia watu akiwa peke yake alijiua baada ya kufanya shambulio hilo.
Kwa mujibu wa wachunguzi, Vladislav Roslyakov kijana mwenye umri wa miaka 18 ndiye mtuhumiwa mkuu. Inaelezwa kwamba alifika kwenye chuo hicho mchana wa tarehe 17.10.2018 huku akiwa amebeba silaha na kisha kuanza kufyatua risasi. Mwili wake ulipatikana baadaye ukiwa na majeraha ya bunduki baada ya kujipiga risasi yeye mwenyewe.
Hakuna dalili za haraka zinazoashiria sababu ya kufanyika kwa shambulio hilo, ambalo lilikumbusha mashambulio ya aina hiyo yaliyowahi kufanyika nchini Marekani ambayo wanafunzi walihusika katika kuwashambulia wanafunzi na watu wengine kwenye shule.
Wengi wa walioathirika kutoka ni vijana wanafunzi ambao walipata majeraha ya risasi. Wanafunzi na wafanyakazi katika chuo hicho wameelezea kwamba tukio hilo lilikua la kutisha, wanafunzi walijaribu kukimbia kutoka kwenye jengo hilo.
Rais wa Urusi Vladimir Putin, katika mkutano huko kusini mwa mji wa mapumziko wa Sochi na mwenzake wa Misri, aliwataka wote wanyamaze kimya kwa dakika chache ili kuwakumbuka wote walioathirika. Putin amesema shambulio hili litachunguzwa kwa makini.
Urusi ililikata jimbo la Crimea kutoka Ukraine mnamo mwaka 2014, hatua iliyosababisha lawama kutoka kwa jamii ya kimataifa na kufuatiwa na vikwazo dhidi ya Urusi kutoka nchi za Magharibi, lakini tangu wakati huo hakuna vurugu zozote kubwa zilizotokea katika eneo hilo.