VIBURI VYA WACHEZAJI WA KIGENI,VINAVYOVURUGA MIPANGO YA SIMBA NA YANGA.

VIBURI VYA WACHEZAJI WA KIGENI,VINAVYOVURUGA MIPANGO YA SIMBA NA YANGA.

Like
405
0
Saturday, 19 December 2015
Slider

Na Omary Katanga.

Ni jambo la kawaida kuwepo na wachezaji wa kigeni katika Klabu za soka kwenye mataifa mbalimbali,lengo likiwa ni kuongeza ushindani na kutoa changamoto kwa wachezaji wazawa ili nao waongeze juhudi katika usakataji kandanda uwanjani.

Lakini uwepo huo wa wachezaji wa kigeni,unategemea sana uwezo wa kifedha kwa klabu husika kutokana na ukweli kwamba huwa wanalipwa kiasi kikubwa cha mshahara na marupurupu mengine kuliko mchezaji wa ndani,na hii inadhihirisha pia utofauti wa kiuchezaji kati yao.

Klabu za Simba na Yanga zina historia ya aina yake tangu kuanzishwa kwake zaidi ya miaka 80 iliyopita,na kujizolea umati mkubwa wa mashabiki wakubwa kwa wadogo,wake kwa waume,na kutengeneza pia matabaka mawili yanayohasimiana ndani ya dakika 90.

Klabu hizi zinamilikiwa kwa mtindo wa wanachama,mtindo ambao unawanyima uhalali viongozi wake kufanya jambo au kutoa maamuzi makubwa kuhusu klabu yao bila kushirikisha wanachama kupitia mkutano mkuu au mtindo wa kupiga kura kupitia vikao maalumu vinavyoitishwa kwaaajili hiyo.

Lakini mbali na kujitengenezea historia ya aina yake ndani na nje ya nchini,Simba na Yanga pia zina historia ya kufanya usajili wa kuviziana, kuigana na wakati mwingine kukomoana kwa lengo la kuwafurahisha wanachama na mashabiki wao.

Huwezi kushangaa kuona Simba ikisafiri kuelekea nchi jirani mfano Rwanda,Uganda,Kenya,Burundi na kwengineko kusaka wachezaji wa kuwasajili,na wakati huo huo kuona watani wao Yanga nao wakikatiza katika mitaa ya nchi hizo kujaribu kuwazidi kete wenzao.

Hivi karibuni tumeshuhudia Simba ikihangaika kumtuliza mshambuliaji wao wa Mganda Emanuel Okwi aliyekuwa akiwasumbua sana licha ya kumsajili kwa kiasi kikubwa cha fedha,lakini bado viongozi wa Simba waliendelea kumnyenyekea,huku wakitambua kuwa wanawakera mashabiki wao.

Ukiachilia mbali Emanuel Okwi,huko nyuma Simba wamewahi kusumbuliwa sana na wachezaji,Suleiman Ndikumana kutoka Burundi,Emeh Ezechukwu kutoka Nigeria, Felix Sunzi wa Zambia na wengineo kadhaa,waliokuwa wakati mwingine wakijiamulia mambo bila kufuata utaratibu wa klabu.

Kwa upande wa Yanga kwa sasa wanakiona cha moto kutokana na tabia ya kiungo wao Mnyarwanda, Harouna Niyonzima,ambaye naye anautunishia kifua uongozi wa klabu yake,na kujaribu kutunga kila aina ya uongo ili kubariki tabia yake ya utovu wa nidhamu anayoifanya hapa ugenini.

lakini utakumbuka pia miaka ya nyuma Yanga imekumbana na kadhia kama hiyo kutoka kwa wachezaji,Ernest Boakye raia wa Ghana pamoja na mlinda mlango Yaw Berko,ambaye yeye uongozi uliamua kumpa adhabu ya kumuweka benchi mpaka mkataba wake ulipomalizika na kumfungulia mlango wa kutokea.

 

 

Usumbufu huu wa wachezaji wa kigeni,unatibua kwa kiasi kikubwa mipango ya klabu husika na kujikuta ikipata matokeo yasiyoridhisha kwa kuwa wakati mwingine wachezaji hao wanakuwa tegemeo la kocha kwenye kikosi chake cha kwanza.

Nionavyo mimi njia pekee ya kukwepa usumbufu huu,ni vilabu kuongeza kasi kwa kuwainua,kuwaamini na kuwapa nafasi wachezaji chipukizi kwenye vikosi vyao vya pili,ili kujiwekea hazina ya baadaye kwenye vikosi vyao vya wakubwa,na kuachana kabisa ulimbukeni wa kukimbilia nje kutafuta wachezaji wanaowatia hasara na kuvuruga mipango yao kila mwaka.

MWISHO.

 

Comments are closed.